• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:50 AM
UFUGAJI: Mbuzi wamemfungulia milango ya kulipa karo

UFUGAJI: Mbuzi wamemfungulia milango ya kulipa karo

NA JOHN NJOROGE

WAKATI Harrison Simotwo alihamia boma lake jipya 1996 kutoka Baringo Kaskazini, alianza kufuga ng’ombe wa maziwa na kondoo ili kujimudu kimaisha.

Baada ya miaka kadha, mkulima huyu mdogo wa kutoka kitongoji cha Silanga eneo la Mau Summit, Kuresoi Kaskazini katika Kaunti ya Nakuru aliamua kufuga mbuzi wa maziwa aina ya Alpine kwa matumizi ya nyumbani na pia kuuza.

“Kwa Sh12,000 nilizokuwa nazo baada ya kuuza kondoo watatu, nilinunua mbuzi mmoja aina ya Alpine kutoka kwa mkulima wa mtaa kwa Sh11,000,” akasema na kuongeza kuwa kwa Sh30,000 alizokuwa nazo kwa ujumla, alijenga muundo rahisi wa kuweka mifugo yake.

Simotwo, 62, alisema kuwa mbuzi huyo aliyekuwa na mimba alizaa mapacha baada ya miezi miwili.

Aliuza baadhi ya kundi lake la kondoo na kuongeza mbuzi zingine ingawa alikumbana na changamoto ya kupata mfugo aliyefaa kwani alitumia mbuzi dume wa kuajiri kutoka kwa wakulima wenzake.

Simotwo hulisha mbuzi wake katika jengo lililoinuka ambalo humsaidia kuwalisha katika mazingira safi.

“Kwa kuinua muundo huu, mbuzi hupata nafasi nzuri wakati wa kula bila kukanyaga unyevu ambao huathiri miguu yake. Muundo huu hunipa nafasi nzuri ya kutoa mbolea kwa urahisi,” akasema.

Yeye hana majuto tangu alipopunguza kundi lake la ng’ombe akisema amenufaika zaidi tangu alipoanza kufuga mbuzi.Mbolea ya wanyama humsaidia hasa wakati bei ya mbolea sokoni imekuwa chache ama ghali.

“Ilikuwa changamoto kuuza maziwa kwa chama cha ushirika kwa sababu bei ilikuwa chini. Niliuza baadhi ya ng’ombe wangu kwani gharama ya kuwalisha iliongezeka,” akasema.

Mbuzi hawa hupunguza gharama ya malisho. Wanakula chochote kilicho cha kijani bila kutumia chakula maalam.

Ili kuwapa hali nzuri ya kiafya,huwapa mbuzi wake dawa ya minyoo mara kwa mara.

Yeye hulipa karo kupitia ukulima huu na kuwaomba wakulima kufuga mbuzi hizi kwa wingi ili kufaulu kimaisha. Alisema maziwa ya mbuzi ni bora; huwa na virutubisho ikilinganishwa na maziwa mengine.

Lita moja ya maziwa ya mbuzi huuza kati ya Sh150 na Sh200 ikilinganishwa na Sh50 kwa maziwa ya ng’ombe.

“Bei ya maziwa huwa na soko nzuri. Nawasihi wakulima kukumbatia ufugaji huu,” akasema.

Mbuzi wa Alpine aliyekomaa huuza kati ya Sh15,000 na Sh25,000.

Harrison Simotwo, 62, akikagua mbuzi wake wa maziwa aina ya Alpine eneo la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru. PICHA | JOHN NJOROGE

Simotwo huelimisha wakulima wengine na kuwahimiza kufuga mbuzi wa maziwa. Ana matumaini ya kuwa mzalishaji wa mifugo ya kiwango cha juu huku akifuga mbuzi 200 ama zaidi kila mwaka.

Ameiomba serikali kupitia idara ya mifugo kuwapa mifugo bora na kuwatafutia soko nzuri ili wasiwe wakiuza maziwa yao kwa soko la ndani.

“Maafisa wa serikali na mashirika yasiyo ya serikali wafaa kuwatembelea wakulima wote bila ubaguzi na kuwapa mafunzo ya kufaa,” akasema na kuwahimiza walio na rasilimali serikalini kuzidi kuwapa mbuzi bora, kufungua viwanda vya maziwa ili kuongeza uchumi wa nchi.

Simotwo hupata mafunzo kupitia mitandao, maonyesho ya kilimo na mashirika mengine yasiyo ya serikali ambayo humfaidi pamoja na wakulima wenzake.

Anapanga kufuga mbuzi kupitia teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji.

Ofisa wa mifugo katika eneo hilo Antony Kariuki amewahimiza wakulima kukumbatia ukulima huu kwa vile ni rahisi kufuga ikilinganishwa na ule wa mifugo wengine.

Alisema kiasi cha chakula ambacho ng’ombe mmoja hula,huliwa na mbuzi sita kwa wakati mmoja!

“Tunawahimiza wakulima kuwapa mifugo wao dawa za minyoo baada ya miezi mitatu na kupanda mazao ya lishe kwa wingi. Pia kuwapa mifugo yao vitamini kupitia sindano au kuchanganya kwa chakula, na kuwapa chumvi lick ambayo huongeza madini mwilini,” akasema Kariuki na kuongeza kuwa chanjo ni muhimu kwa mifugo.

  • Tags

You can share this post!

Ni muhimu kupunguza matumizi ya sukari nyeupe

ZARAA: Makadamia yalishuka bei 2020, uongezeaji thamani...

T L