• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:55 PM
IEBC yatoa mapendekezo kadhaa yanayolenga kuboresha uchaguzi mkuu wa 2027

IEBC yatoa mapendekezo kadhaa yanayolenga kuboresha uchaguzi mkuu wa 2027

NA CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imependekeza hatua kadha na mahitaji ambayo yanapaswa kutimizwa kufanikisha uchaguzi mkuu ujao wa 2027.

Kulingana na ripoti yake kuhusu tathmini ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, tume hiyo inasema panahitajika mageuzi ya kisheria, kutolewa mapema kwa fedha za kufadhili shughuli za uchaguzi, ununuzi wa vifaa hitajika mapema, kuanzishwa kwa hazina maalum ya IEBC miongoni mwa hatua nyinginezo.

Ripoti hiyo kwa jina, “The Post Election Evaluation Report for the August 9, 2022 General Election” pia inapendekeza kuteuliwa kwa makamishna wa IEBC angalau miaka miwili kabla ya tarehe ya uchaguzi, kutolewa kwa mafunzo maalum kwa wafanyakazi wa tume na wadau muhimu na ujenzi wa makao makuu ya tume.

Aidha, ripoti hiyo iliyozinduliwa katika mkahawa wa Safari Park mnamo Jumatatu, Januari 16, 2022 inapendekeza kuimarishwa kwa mfumo wa upeperushaji wa matokeo kutoka kwa vituo vya kupigia kura hadi katika vituo vya kujumlisha kura katika maeneo bunge na kituo cha kitaifa.

“Sheria muhimu za kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi huru na zinahitajika kupitishwa mapema sawa na ufadhili tosha kutolewa ili kufanikisha usajiliwa wapiga kura wapya mapema, ununuzi wa vifaa hitajika na uajiri wa wafanyakazi ni muhimu kwa ufanikishaji wa uchaguzi wa huru na haki,” ripoti hiyo inasema.

Baadhi ya miswada ambayo IEBC inataka ipitishwe na bunge ili kuboresha kufanyika kwa uchaguzi ni; Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi, Mswada kuhusu Ufadhili wa Kampeni, Mswada wa Marekebisho ya Sheria za IEBC, 2020 na Mswada wa Kura ya Maamuzi wa 2022.

Pendekezo muhimu katika mswada wa marekebisho wa sheria za uchaguzi ni uoanishaji wa sheria hiyo na Sheria mpya ya Vyama vya Kisiasa kufanikisha kufanyika kwa mchujo mzuri na kusuluhishwa kwa mizozo ibuka.

Miswada hiyo iliwasilishwa bungeni na IEBC katika bunge la 12 lakini haikupitishwa na wabunge.

Kwenye ripoti hiyo, IEBC pia inapendekeza kuwa Katiba ifanyiwe marekebisho ili kutenganisha chaguzi za viti vya kitaifa na chaguzi za viti vya kaunti.

Viti vya kitaifa ni; urais, ubunge na useneta ilhali viti vya kaunti ni ugavana na udiwani.

“Kuendeshwa kwa chaguzi sita mara moja siku moja huweka presha kwa maafisa wa uchaguzi hivyo kuwafanya kuchoka kutokana na kazi nzito. Hali hii huenda ikachangia baadhi yao kufanya makosa wasiyoyakusudia,” ikasema ripoti hiyo iliyozinduliwa katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi.

IEBC pia inasema ingependa kuimarisha ujumuishaji wa wote katika mchakato wa uchaguzi kwa kutoa vifaa vitakavyowawezesha watu wanaoishi na uelemavu kujisajli na kupiga kura.

“Vifaa hivyo ni kama vile, maeneo maalum ya kupigia kura, karatasi za kura zilizotengenezwa kwa mfumo wa braili na vifaa maalum kuwa kuwawezesha kusikia na kuhisi,” ikasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo ilizinduliwa na mwenyekiti mstaafu wa IEBC Wafula Chebukati, akiandamana na makamishna wa zamani Abdi Guliye na Boya Molu.

Huenda mapendekezo hayo yakaongeza gharama ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, IEBC ilitoa bajeti ya Sh40.9 bilioni, ambayo ilisawiriwa kuwa kubwa zaidi ishara kuwa uchaguzi wa Kenya ni ghali mno.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Makadamia yalishuka bei 2020, uongezeaji thamani...

CHARLES WASONGA: Machifu, Nyumba Kumi walinde wazee...

T L