• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
ZARAA: Matomoko ni yenye thamani kubwa kwake

ZARAA: Matomoko ni yenye thamani kubwa kwake

NA SAMMY WAWERU

KIJIJI cha Nyati, Kamahuha, Murang’a ni chenye shughuli tele, ukuzaji wa maparachichi, maembe na ndizi ukishika kasi.

Wenyeji pia wanalima mahindi na maharagwe.

Katika shamba la Frdrick Kinyanjui, amejumuisha mseto wa matunda hayo ila ana utofauti wa kipekee.

Akiwa na zaidi ya ekari sita, nusu ikiwa uga wa ndizi aina ya plantain kati amepanda matunda aina ya matokomo.

Ni zao la thamani linaloendelezwa na wakulima wanaohesabika nchini.

Mzee Kinyanjui ni mmoja wao, na ana jumla idadi ya miti 39 inayozalisha.

Kati ya matunda anayolima, anafananisha matomoko na dhahabu.

Anafichua kwamba alirithi kilimo hicho kutoka kwa babake 1995.

“Alianza kulima matomoko miaka ya 70,” adokeza.

Matunda hayo matamu, ni ya kijani na yenye ngozi iliyoparara yakienziwa kufuatia virutubisho vyake kiafya.

Kinyanjui alikuwa dereva wa matrela ya masafa marefu, na anakiri hajutii kuacha kazi hiyo kuendeleza ukuzaji wa matomoko.

Ni baba wa watoto watatu wote wakikata kiu cha masomo kupitia kilimobiashara cha matunda hayo.

Mmoja tayari, ameonyesha dalili za kurithi jitihada zake.

“Nilikuwa nimehudumu kama dreva wa matrela miaka 22,” afichua.

Hata ingawa Kinyanjui hakumbuki idadi ya miti aliyorithi, anasema alilazimika kung’oa mikahawa kwa kile anataja kama “mahangaiko aliyopitia kwa sababu ya bei duni ya kiungo hicho cha kinywaji”.

Alichukua hatua hiyo, wakati ambapo sekta ya kahawa haikuwa imeanza kutekelezwa mageuzi.

Anasifia matomoko, akisisitiza yalifuta changamoto alizopitia.

Mkulima huyu wa haiba yake, hukuza aina ya soursop.

Hujamiisha, kupitia mfumo wa kupandikiza kupata yaliyoboreshwa.

Anaambia Akilimali kwamba hutoa mbegu maeneo ya Ukambani na Meru – Matomoko asilia.

“Baada ya kupata miche ya kienyeji, huipandikiza na matawi ninayolima kupata iliyoboreshwa,” aelezea.

Uchipukaji wa mbegu asilia, Kinyanjui anasema ni karibu asilimia 100.

Ana kitalu cha shughuli hiyo.

Kulingana na Meshack Wachira ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kilimo, mbegu zinapaswa kuwa za mtomoko ulionawiri na kuwa huru dhidi ya magonjwa na wadudu.

“Isitoshe, matunda yanayotumika kupata mbegu yawe yaliyokomaa na kuifa vizuri,” ashauri mdau huyo.

Kulingana na mkulima Kinyanjui, miaka sita baada ya upanzi miche iliyopandikizwa huanza kutunda.

Muhimu, ni kutunza mitomoko kwa mbolea, fatalaiza na maji.

Ana dimbwi la maji, na vilevile ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi na kuku.

Hali kadhalika, huzalisha nguvu za kawi kwa kinyesi cha ng’ombe ambacho pia hukielekeza shambani kunawirisha matunda.

Septemba, mitomoko huangusha majani yote kubisha hodi msimu wa maua kuchana Oktoba na kuanza kutunda.

“Kipindi hicho yanahitaji maji kwa wingi,” Kinyanjui asisitiza.

Mazao mengi hushuhudiwa kati ya Aprili na Agosti, mwezi Oktoba yakiwa haba.

Wastani, mti mmoja unazalisha hadi kilo 700 kwa mwaka.

Kinyanjui anasema kilo moja haipungui Sh80 bei jumla ya langoni – shambani.

Ameanza kuandamwa na wauzaji wa matunda ng’ambo, akisema kilo moja inavutia zaidi ya Sh100.

Kero ya magonjwa ni haba, wadudu anaoshuhudia wakiwa nzi wa matunda na False Codling Moth.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa wafanyikazi, akilalamikia vijana kutekwa nyara na pombe.

  • Tags

You can share this post!

Roho mkononi Simbas wakisubiri kambi ya mazoezi raga SA

Maafisa watatu wa zamani wa Tana River washtakiwa mjini...

T L