• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
ZARAA: Minazi si ya Pwani pekee, yaweza kuwa pato kwa ‘watu wa bara’

ZARAA: Minazi si ya Pwani pekee, yaweza kuwa pato kwa ‘watu wa bara’

NA LABAAN SHABAAN

TAKWIMU za Wizara ya Kilimo 2021, zinaonyesha nazi huzalishwa katika kaunti sita za pwani; Kilifi, Kwale, Lamu, Mombasa, Taita Taveta na Tana River.

Ila kuna uwezo mkubwa kwa kaunti nyingine kama Tharaka Nithi, Meru, sehemu kadhaa Makueni, Machakos, Busia, Homa Bay na Siaya kuzalisha mazao ya minazi nchini.

Kenya ina uwezo wa kuzoa Sh25 bilioni kila mwaka kutoka kwa minazi ila ni asilimia 53 pekee inatekelezwa.

Hali hii inadhihirisha kuwa uwezo wa asilimia 47 wa nchi kukuza minazi bado haujakumbatiwa na kunyima Kenya mapato ya zaraa yanayohitajika kuafikia malengo endelevu ya maendeleo.

Mzee Richard Koisia, 78, ni mkulima wa minazi ambaye ni mfano maridhawa wa kuonyesha dhahiri kilimo hiki kinastawi eneo la Mwani, kaunti ndogo ya Kaiti, Kaunti ya Makueni.

Ana shamba la ekari 34 lenye mamia ya minazi.

Akilimali inapomkuta shambani mwake, anatuchorea taswira na kukumbuka mwaka wa 1984 alipohudhuria warsha Mombasa ambayo ilibadilisha mkondo wa maisha yake.

“Nilirejea na nazi nne, tukala tatu na moja nikapanda vivi hivi tu nikasahau. Baada ya mwaka mmoja nikapitia hapo nikaona imemea nikashangaa! Ni baada ya miaka 20 ambapo niliona maua mara ya kwanza,” Koisia anasema.

“Mimi sikusoma. Nilikuwa naangalia umbali wa kila mnazi kutumia macho nikiwa Mombasa kisha narejea Makueni kupanda. Nilinunua miche inayofaa nilipogundua minazi inamea Makueni,” anaongeza.

Yeye ni mkulima wa kipekee wa minazi katika sehemu pana ya kaunti ndogo ya Kaiti ambapo pamejaa wakulima wa matunda, viazi vitamu na kadhalika. Anatuarifu wakulima hustaajabia chaguo lake la kilimo.

“Baada ya watu wa Makueni kuona minazi inamea kwangu, wakaanza kuniuliza na kufikia sasa nimeuza miche 700 na ninafurahi sana naendeleza kilimo ambacho hakikujulikana hapa tangu zamani,” Koisia anasema.

“Si hapa kwangu tu inaweza kumea. Sehemu nyingine Makueni inawezekana. Wakulima wengi hawajui na wengine hawataki,” anaongeza.

Safari ya zaidi ya miaka 30 ya Mzee Koisia katika ukuzaji wa minazi ilikuwa na changamoto tele.

Miaka ya tisini kuna wakati alienda Mombasa na kurudi kujaribu kupanda halafu miche yote ikaoza na kuharibika.

Alipata maarifa kutoka kwa wakulima wengine waliomwonyesha mbinu za upanzi zilizokomaza minazi kwa miaka kumi. Koisia alipokutana na watalaamu walimfunza mitindo ya kupanda na spishi zinazokua kwa miaka mitano.

“Nilipoanza kuandaa miche ilinichukua miaka mitatu ili nifaulu kuotesha kitalu. Nilikuwa napanda 10 zote zinaoza ama moja inamea kwa sababu nimeweka vibaya. Baada ya pata potea zangu nikafaulu, nikipanda 10 zinamea nane.”

Changamoto yake kubwa ni wezi ambao aghalabu huiba usiku ila hii haikudhihirika kama inamsumbua sana. Anachoshughulikia kwa karibu ni kuhakikisha minazi haiathiriwi na vimelea kwa kunyunyiza dawa na mara kwa mara kutalii shambani kujua matatizo.

Mzee Koisia huuza nazi kwa wateja wa matumizi ya nyumbani na wanabiashara kwa Sh40.

Anatufahamisha kuwa hawezi kutosheleza mahitaji hivyo kuna haja ya wakulima wengine kuchangamkia kilimo hiki.

“Kila siku nauza nazi takriban hamsini. Pia ninauza fagio na siwezi kutosheleza oda kwa sababu huwa nyingi. Vile vile nauza miche kwa Sh500 kila mmoja,” Koisia anasema.

Minazi ni uwekezaji wa miaka mingi. Kabla ya Makueni kuorodheshwa kiutalamu kama eneo faafu la ukuzaji minazi, Mzee Koisia alijaribu bahati na kufaulu licha ya changamoto.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Suala la jisia halifai kutumika na IEBC...

Maskwota wa Mavoloni wataka usaidizi kutoka kwa serikali

T L