• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Maskwota wa Mavoloni wataka usaidizi kutoka kwa serikali

Maskwota wa Mavoloni wataka usaidizi kutoka kwa serikali

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Mavoloni, Yatta, kaunti ya Machakos, wametoa malalamiko baada ya kufurushwa kutoka maeneo ya milimani walikokuwa wakiishi kwa miaka mingi.

Familia zaidi ya 300 zilifurushwa wiki jana, kutoka maeneo hayo ambayo wameishi kwa miaka mingi.

Baada ya kutimuliwa mahali hapo sasa maskwota hao wamelazimika kutafuta makazi mapya katika makanisa na vijiji vilivyoko karibu na mahali hapo.

Tayari wameanza kuchukua saini wakilalamika kwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) ili kuingilia kati.

Baada ya kufurshwa, eneo hilo liligeuzwa eneo la uchimbaji wa mawe na madini.

Tayari wakazi wa Mavoloni waliofurushwa wameanza kuchukua saini wakilalamika kwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) ili kuingilia kati. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Mwenyekiti wa maskwota chini ya mwavuli wa Ndalani Squatters Association Bw Francis Kilango, alisema wale waliowafurusha wangefuata utaratibu uliostahili wa kuwahusisha wakazi wa kijiji hicho katika mazungumzo.

“Kikundi cha watu binafsi waliowafurusha wakazi hao walichukua sheria mikononi mwao kwani hawakuzungumza nao ilivyotarajiwa, bali walifika na fujo na kuwaondoa,” aliteta Bw kilango.

Alisema tayari anafanya juhudi kuchukua saini za wakazi wapatao 300 ili kuwasilishwa kwa serikali kulalamikia kile anachokiita ni ukiukaji wa haki za binadamu.

Aliiomba NLC kuingilia kati ili kubainisha ukweli wa mambo.

Alisema wakazi hao waliofurushwa wamepitia masaibu mengi hata tayari wengine wameathirika kiafya hata wakafa kutokana na msongo wa mawazo tele.

Naye Wambua Nzau, alisema kabla ya wakazi hao kufurushwa hakuna majadiliano yoyote yaliyofanyika

Alisema tangu wakazi hao kufurushwa mahali hapo wiki chache zilizopita wengi wa wazee wameugua huku wengine wakipoteza maisha yao kwa kushtuka.

“Ninatoa wito kwa afisa mkuu wa upelelezi kutoka Machakos achukue jukumu kuona ya kwamba uchunguzi kamili unafanywa ili kuwachukulia hatua kali watu wale waliowafurusha wakazi hao,” alifafanua Bw Nzau.

Alitoa mfano wa mzee mmoja Bw Francis Waithaka ambaye alipata majeraha ya risasi polisi walipokuwa wakiwaondoa eneo hilo.

Wakazi hao wanataka Rais Uhuru Kenyatta, kuingilia kati kuona ya kwamba wanaruhusiwa kurudi kwa makazi yao ama watafutiwe eneo lingine.

Askofu wa eneo hilo Bw Hosea Nthimba na Bi Jane Kanini waliohojiwa walisema hali ya maisha kwa wakazi hao ni ngumu ajabu ambapo wanastahili kuokolewa haraka iwezekanavyo.

Walisema wale walioathirika zaidi ni wanawake na watoto wadogo kwa sababu hawana makazi maalum na chakula cha kuwakimu.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Minazi si ya Pwani pekee, yaweza kuwa pato kwa...

TAARIFA ZA WIKI: Kumbatieni lishe ya wadudu kupambana na...

T L