• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
ZARAA: Ushawazia mahindi ya zambarau? Mdau anasisitiza yanalipa

ZARAA: Ushawazia mahindi ya zambarau? Mdau anasisitiza yanalipa

NA PETER CHANGTOEK

WAKULIMA katika maeneo mengi nchini, hupenda kuzalisha mahindi yaliyo na rangi nyeupe kwa ajili ya kupata lishe na riziki.

Hata hivyo, mkulima mmoja katika Kaunti ya Bungoma aliamua kuchukua mkondo tofauti.Gentrix Naliaka Maindi, anasema kuwa, mahindi yaliyo na rangi ya zambarau yana faida tele na virutubisho muhimu mwilini, yakilinganishwa na yale meupe.

“Mimi hukuza mahindi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Hata hivyo, 2017 nilipata wazo la kukuza mahindi ya kiasili ambayo mamangu amekuwa akikuza kwa ajili ya kuliwa nyumbani, ambayo hujulikana kama ‘Makondo’ au ‘Namba nane’,” asema.

Alipoanza, alikuwa akilitumia shamba robo ekari. Hata hivyo, anasema kuwa, ametumia mtaji wa Sh100,000 mwaka huu kwa shamba ekari tatu.

“Kwanza, nilianza kukuza kwa sababu ni asilia. Pili, ni kwa sababu yana faida kuliko yale yenye rangi nyeupe. Nilipendezwa na mahindi hayo ya zambarau na nikachagua mbegu na kuzipanda peke yake,” adokeza.

Mkulima huyo anadokeza kuwa, wengi wa kizazi cha sasa hawajui kuhusu mahindi hayo ya kiasili. Hata hivyo, anasema yana manufaa kwa afya ya binadamu.

“Ni lishe kuu, ambayo husaidia kuimarisha kinga mwilini dhidi ya magonjwa. Pia, ni faafu kwa wale wanaougua maradhi ya mitindo ya maisha kama vile shinikizo la damu, matatizo ya moyo, kisukari na walio na uzito kupindukia. Pia, yasemekana kuwa yana uwezo wa kuzuia ugonjwa wa kansa,” afichua Maindi.

Mkulima huyo anaongeza kuwa, mahindi hayo hutumika katika shughuli ya uokaji kuongeza rangi asilia na katika viwanda vya kutengeneza vyakula.

Anasema kwamba ni yeye tu katika eneo hilo, anayeyazalisha mahindi ya zambarau na kwamba huyapenda sana mahindi yayo hayo.

Anafichua kwamba, hulima shamba mara mbili kabla hajazipanda mbegu.

Hutumia mbolea za DAP, CAN na NPK kwa ukuzaji wa mahindi hayo. Hata hivyo, anasema kuwa, anapania kuanza kutumia mbolea asilia.

“Huchukua miezi sita kukomaa. Hata hivyo, yakiwa na miezi minne, unaweza kuchemsha na kula,” asema Maindi.

Kuna baadhi ya changamoto ambazo amewahi kupitia katika shughuli hiyo. Wakati mwingine kuna wadudu wanaovamia mahindi shambani.

Aidha, ukosefu wa mvua hufanya baadhi ya mbegu kukosa kuota. Pia, ukosefu wa pembejeo za kutosha ni changamoto kwa mkulima huyo. Isitoshe, anasema kuwa, watu wengi wamezoea mahindi meupe, na hivyo huchukua muda kuzoea yale ya zambarau.

Shida nyingine ni kuwa, ndege huvamia mahindi shambani na baadhi ya watu huyaiba shambani. Hata hivyo, changamoto hizo hazijamzuia kuendeleza kilimo hicho.

Maindi anasema kuwa, anapania kuanza kuongeza thamani kwa mahindi hayo kwa kutengeneza unga wa uji, ugali na unga wa kuokea mikate na keki.

“Unga huo utawalenga wale walio na magonjwa yanayosababishwa na mitindo ya maisha na wale wanaotaka kula lishe bora,” aongeza.

Mkulima huyo anafichua kuwa, ananuia kutengeneza sharubati ya unga wa mahindi ya zambarau, anasema hupatikana sana nchini Peru, ijulikanayo kama Chira Morada.

Kwa mujibu wa mkulima huyo ni kwamba, mahindi hayo ya zambarau huuzwa kwa bei ghali ikilinganishwa na yale meupe.

“Najua waagizaji wanaoyauza kwa Sh1,500 na zaidi,” asema Maindi, akiwashauri watu waanze kujitosa katika ukulima huo.

Anasema kwamba, ukuzaji wa mahindi hayo utawafaa mno watu kuhakikisha kuwa kuna utoshelevu wa chakula nchini. Aidha, anasema kuwa mahindi hayo yatatia pesa nyingi mifukoni mwa wakulima ikilinganishwa na mahindi meupe.

  • Tags

You can share this post!

Rais mteule azungumza na Rais anayestaafu

DARUBINI YA WIKI

T L