• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
ZARAA: Wavutia soko la ng’ambo kwa mboga zilizokaushwa

ZARAA: Wavutia soko la ng’ambo kwa mboga zilizokaushwa

NA SAMMY WAWERU

ENDAPO kuna kilimo kilichokumbwa na uharibifu wa mazao ni ukuzaji wa mboga.

Si ajabu shambani ukishuhudia mkulima akilisha mifugo mazao yake, na mengine kuozea migundani ilhali mijini yameadimika.

Kwenye majaa ya soko, taswira hiyo si tofauti – mboga kuoza kwa sababu ya kukawia na kukosa wanunuzi.

Licha ya changamoto hizo, ulijua zinaweza kuongezwa thamani kwa kukausha zitumike wakati wa majanga?

Hilo linawezekena, na mfumo huo ukikumbatiwa itakuwa afueni kwa wazalishaji ambao ni wakulima na wauzaji.

Mace Foods Ltd, kampuni yenye makao yake makuu Eldoret inajituma kuangazia gapu hiyo kwa kukausha mseto wa mboga.

Kuanzia managu – mnavu, sukuma wiki, saga na kunde, Tedyline Murylah ambaye ni Meneja Mkurugenzi wa Mikakati anasema mtandao wa uongezaji thamani mboga hizo haujaangaziwa vilivyo.

Kampuni hiyo vilevile husindika pililili hoho yaani zile kali.

Inalenga soko la ndani kwa ndani na ng’ambo, ikiwa na kiwanda cha ukaushaji katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Kulingana na afisa huyo, wakati wa mavuno vigezo kadha wa kadha vinazingatiwa.

Mosi, mboga zinachumwa kwa mikono, aina na rangi ya majani ikipewa kipau mbele.

Aidha, majani yanapaswa kuwa katika hali bora, yaliyochana maua na matunda yanaondolewa.

“Yanapitishwa kwenye maji moto kwa muda mfupi (blanching),” Tedyline asema.

Tedyline Murylah (kushoto), Meneja Mkurugenzi wa Mikakati Mace Foods Ltd na Anita Jeptoo, Meneja Msimamizi masuala ya Wateja wakionyesha mseto wa mboga zilizoongezwa thamani, wakati wa maonyesho yaliyoandaliwa na Wadauhusika Sekta ya Kibinafsi katika Kilimo (ASNET) 2022, makao makuu ya Kalro, Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Baadaye, mazao hayo huwekwa kwenye mashine za joto kisha kukaushwa ili kuondoa unyevu wa maji yaliyosalia.

“Kinachofuata, ni kuyapakia tayari kuingia sokoni,” aelezea.

Tedyline anaambia Akilimali pakiti ya kilo 50 bei jumla ni Sh50, bidhaa zilizoongezwa thamani zikifika sokoni kama vile maduka ya kijumla inachezea Sh225 – 300.

Ikiwa ilizinduliwa 2004 na kujiunga na mtandao wa uongezaji mboga thamani miaka miwili baadaye, afisa huyo anafichua Mace Foods Ltd inahudumu katika kaunti 14 nchini.

Anadokeza kwamba kwa sasa ina idadi jumla ya wakulima 2, 471 wanaokuza mseto wa mboga na wengine pilipili hoho.

“Tunashirikiana na Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis), kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zilizoafikia ubora wa bidhaa,” Tedyline afafanua, akisisitiza wanahamasisha wakulima kukuza mboga za kienyeji kwa kile anataja “zinateka soko lenye ushindani mkuu hasa ng’ambo”.

Isitoshe, kampuni hiyo inashiriki katika hatua zote za uzalishaji, kuanzia usambazaji wa mbegu, kulima, matunzo ya mimea, mavuno, usindikaji na masuala ya soko.

Kulingana na mashirika yanayotafutia wakulima wanunuzi nje ya nchi, mazao yaliyoongezwa thamani yanateka masoko yenye ushindani mkubwa.

“Chini ya asilimia 10 ya mazao tunayouza ng’ambo ndiyo huwa yameongezwa thamani, na yanateka mapato karibu mara tatu ya yale mabichi,” adokeza Kate Nkatha, Mkurugenzi Mkuu wa Mauzo Fairtrade Africa.

Matumizi ya mifumo ya kisasa katika kilimo, ni kati ya vigezo wakulima wanahimizwa kukumbatia ili kuboresha mazao.

Kujiunga na Mace Foods Ltd, mkulima hupigwa msasa kwa mujibu wa eneo aliko, kiwango cha shamba kikipaswa kuwa zaidi ya ekari moja na vilevile chaguo la mboga.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Ukakamavu umemuinua katika uuzaji wa mitumba

BI TAIFA JULAI 27, 2022

T L