• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 2:55 PM
UJASIRIAMALI: Ukakamavu umemuinua katika uuzaji wa mitumba

UJASIRIAMALI: Ukakamavu umemuinua katika uuzaji wa mitumba

NA PETER CHANGTOEK

STACY Auma alikuwa akifanya kazi ya kuchuuza nguo katika maeneo tofauti tofauti nchini, kabla ya kufanikiwa na kuanza kuagiza mitumba kutoka ughaibuni na kuuza nchini.

Hata hivyo, alikuwa akifanya shughuli nyingine kabla ya ufanisi kubisha hodi.

“Nilikuwa nikiwafulia watu nguo katika eneo la Greenspan. Lakini ilifika wakati ambapo nisingefanya hivyo kwa sababu ya maumivu ya mgongo. Mama yangu akanishauri nianzishe biashara ya kuuza chakula, nikaanza kuuza samaki,” asimulia Auma.

Baada ya kuuza samaki kwa muda wa miezi minne, biashara hiyo ilimlemea kwa sababu ya changamoto kadha wa kadha.

Mama yake akamshauri aende Gikomba ili ajue ni nguo zipi ambazo hupendwa sana, ili aanzishe biashara ya kuuza nguo.

“Nilikuwa na Sh500 na mama yangu akaniongezea Sh500. Nikanunua sweta 30 kwa Sh30 kila moja na kuzipeleka kupigiwa pasi kwa Sh2 kila moja,” anasema, akiongeza kuwa, alianza kuzitembeza akiziuza katika saluni na sehemu tofauti tofauti.

Auma alikuwa akiziuza kwa Sh100 ambapo alikuwa akipata faida ya takribani Sh70 kwa kila moja.

“Siku moja nilipatana na rafiki yangu ambaye nilikuwa nikisoma naye, akiuza bidhaa jijini, akaniambia niende nijaribu huko,” adokeza.

Hata hivyo, alitiwa mbaroni na askari wa kaunti, almaarufu kanjo.

Walimtia mbaroni saa kumi na kumwachilia saa tatu usiku. Ilimbidi ampigie simu mama yake amtumie nauli kwa sababu hakuwa ameuza kitu.

Hata hivyo, hakufa moyo. Siku ya pili alirudi jijini tena na kwa bahati nzuri, akauza nguo zote. Katika siku ya tatu, akatiwa mbaroni tena.

Mchezo wa paka na panya uliendelea baina yake na kanjo, jambo lililomfanya awaze na kuwazua.

Baadaye, aliamua kuanzisha shughuli ya kuuza mitumba katika eneo la Gikomba.

Ili kuagiza mitumba ughaibuni, alilazimika kuwa na Sh1 milioni, hela ambazo hakuwa nazo.

Ilibidi waungane na watu wengine, ili kila mmoja atoe Sh200,000.

“Mamangu aliomba mkopo kutoka kwa akaunti yake, nami nikakopa kutoka kwa akaunti yangu. Kuna mtu aliyeniongezea pesa,” afichua mfanyibiashara huyo.

Hapo ndipo ufanisi wake ulipoanza kuonekana. Kwa sasa, ana duka la kuuzia marobota ya nguo katika eneo la Gikomba. Aidha, ana duka la nguo katika eneo la Roysambu.

“Tuna marobota kutoka Uingereza na Canada,” afichua Auma, ambaye hujulikana kama Stacy wa Mitumba kwa Facebook, jukwaa analolitumia kuziuza bidhaa zake.

Auma pia huwapa ushauri wale wanaonuia kuanzisha biashara ya kuuza nguo. Hata hivyo, kuna changamoto kadhaa katika biashara hiyo.

Ndaro moja ni kuwa, kuna wakati ambapo robota linaweza kuwa na nguo ambazo haziridhishi.Mbali na kutumia Facebook kuziuza bidhaa zake, yeye pia huuza kupitia kwa Instagram, ambapo hujulikana kama Auma Stacy.

Mioto ya kila mara katika soko la Gikomba pia huwaathiri wafanyibiashara wengi.

Auma, ambaye pia ni kocha wa timu mbili za vijana, anadokeza kuwa, katika biashara, utunzaji wa rekodi ni muhimu mno.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Kenya yapunguza uagizaji sukari uzalishaji...

ZARAA: Wavutia soko la ng’ambo kwa mboga zilizokaushwa

T L