• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
BENSON MATHEKA: Serikali isake magenge yote hatari kote nchini jinsi inavyofanya kwa ‘Confirm’

BENSON MATHEKA: Serikali isake magenge yote hatari kote nchini jinsi inavyofanya kwa ‘Confirm’

NA BENSON MATHEKA

HATUA ya waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kutuma kikosi spesheli cha maafisa wa polisi kusaka wanachama wa genge la wahalifu linalojiita ‘Confirm’ katika Kaunti ya Nakuru inafaa hasa ikizingatiwa kuwa wakazi wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu.

Japo waathiriwa wa ukatili wa genge hilo wanahisi kwamba hatua ya serikali imechelewa, ingekuwa muhimu hatua sawa kuchukuliwa katika maeneo mengine ambako wakazi wanahangaishwa na magenge ya wahalifu.

Wakazi wa maeneo mengine ambao wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa usalama miaka nenda miaka rudi lazima wanajiuliza maswali wakihisi kupuuzwa.

Muhimu zaidi kwa wakati huu ni kuhakikisha kuwa maafisa hao wanafaulu katika jukumu lao. Maafisa hao wanapotumwa kukabili magenge, mara nyingi huwa wanashindwa kutokana na ukosefu wa usaidizi wanaohitaji kutoka kwa wakubwa wao hasa wale wa maeneo wanayotumwa kufanya msako.

Hii huwa ni hujuma kwa sababu wakubwa hao huwa wanahisi wanaotumwa wanaingilia kazi yao na huwa wanafanya juu chini wasifaulu.

Ingekuwa jambo la busara kuhakikisha maafisa hao hawawekewi vizingiti katika utelelezaji wa jukumu lao la kukabili na kuangamiza genge hilo la wahalifu ambao msimu huu wa joto la kampeni za uchaguzi mkuu wanaweza kutumiwa na wanasiasa kuvuruga amani.

Nakuru ni mojawapo ya kaunti zilizo katika orodha ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utengamano (NCIC) kama hatari kwa ghasia za baada ya uchaguzi. Hata hivyo, operesheni sawa na aliyoagiza Waziri Matiang’i ifanywe katika kaunti hiyo pia inafaa kufanywa katika maeneo mengine ambako wakazi wanalalamikia ukosefu wa usalama.

Katika msako kama huo, polisi hawawezi kufaulu peke yao, mchango wa wakazi na viongozi unahitajika.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: IEBC itoe maelezo muhimu kuhusu kura mara...

TAHARIRI: Tuchukue tahadhari kuepusha hatari katika kampeni

T L