• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
TAHARIRI: Tuchukue tahadhari kuepusha hatari katika kampeni

TAHARIRI: Tuchukue tahadhari kuepusha hatari katika kampeni

NA MHARIRI

KAMPENI za uchaguzi zimenoga katika kila pembe ya nchi, zikivutia mamia na maelfu ya watu.

Katika hali hii, kila juhudi zinafaa kuwekwa ili kuhakikisha kampeni zote zinafanywa kwa njia salama.

Kwa muda wa miezi michache iliyopita tangu wanasiasa walipoanza kuzidisha kampeni zao, tayari tumeshuhudia visa mbalimbali ambavyo vinatishia usalama wa umma.

Visa hivyo vinajumuisha mikanyagano ya umati, watu kugongwa na magari ya kampeni yanapopinduka au yanapoendeshwa kwa kasi, na pia watu kudandia helikopta zinapopaa kutoka viwanjani.

Kenya huwa ni miongoni mwa nchi kimataifa ambazo zingali zinajitahidi kuwa na kiwango cha kutosha cha walinzi wa usalama wa umma, kwa hivyo, haitakuwa busara kwetu kutarajia polisi watakuwepo kila mara kutudhibiti katika mikutano ya hadhara hasa ya kisiasa kama inavyoshuhudiwa.

Hivyo basi, mbali na mipango ambayo asasi za usalama zimewekea mikutano ya hadhara, ni muhimu pia vyama vya kisiasa na wanasiasa kuchukua hatua zitakazohakikishia wananchi usalama wao wanapohudhuria mikutano ya aina hii.

Kwanza, hili linawezekana kupitia kwa wanasiasa wenyewe kufuata sheria kikamilifu.

Sheria kama vile za uendeshaji magari, idadi ya watu wanaostahili kuwa kwa gari moja au katika eneo moja, sehemu za kupaa na kutua kwa ndege, ni baadhi tu ya zile ambazo zikifuatwa kikamilifu zinaweza kutuepushia mikosi ambayo tumekuwa tukishuhudia katika mikutano ya hadhara.

Idara za serikali zinazohusika katika kudhibiti mambo ya uchukuzi barabarani hazifai kufumbia macho matukio tunayoendelea kushuhudia ambapo magari huendeshwa kiholela hadi kugonga watu au kupinduka ikiwa na watu waliokalia juu.

Kwa msingi uo huo, idara zinazohusika na usimamizi wa safari za ndege za raia hazifai kukaa kando wakati huu wa kampeni ambapo helikopta chungu nzima zinazunguka huku na kule wanasiasa wakiendelea kujitafutia umaarufu.

Nchi hii imekuwa na mazoea ya kusubiri hadi janga kuu litokee kabla hatua mwafaka zichukuliwe, na hilo halifai kuonekana katika maandalizi ya uchaguzi.

Itakuwa busara kama wadau wote husika, sio polisi pekee, watajitolea kuweka mikakati ya kutosha kulinda usalama wa umma katika kipindi hiki kizima cha kampeni za uchaguzi hadi wakati uchaguzi utakapokamilika.

Tusisubiri kuona idadi kubwa ya watu wamefariki ajalini kwa msafara wa kampeni, au tukio la kutisha limeshuhudiwa kabla tuamue kuchukua hatua.

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Serikali isake magenge yote hatari kote...

Urusi yalemewa kulipa madeni yake ya kigeni

T L