• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 8:55 PM
CECIL ODONGO: Raila asiruhusu Azimio la Umoja limeze chama cha ODM

CECIL ODONGO: Raila asiruhusu Azimio la Umoja limeze chama cha ODM

Na CECIL ODONGO

HUKU kampeni za uchaguzi wa Agosti 9, 2022 zikiendelea kushika kasi, miungano mipya inaendelea kusukwa, wanasiasa wakuu wakijiweka pazuri kupigania kiti cha urais.

Chama cha ODM kinachoongozwa na kigogo wa siasa za upinzani Raila Odinga ni kati ya vyama ambavyo vinajipanga kuingia kwenye muungano unaonukia wa Azimio la Umoja.

Katika kampeni zinazoendelea, wanasiasa wa ODM wakiongozwa na Bw Odinga mwenyewe wanaonekana kutomakinikia kuvumisha chama hicho jinsi ilivyokuwa hapo awali.

Badala yake wanasiasa wa ODM wameanza kuweka mikakati ya kujipanga ili kutumia Azimio la Umoja kuwania vyeo mbalimbali, wakionekana kupuuza ‘Chungwa’.

Iwapo mwishowe ODM itaamua kuwasilisha wawaniaji kupitia Azimio la Umoja badala ya chama, basi huenda ikawa sawa na uchaguzi wa 2002 ambapo vyama tanzu ndani ya Narc vilisimamisha wagombeaji ndani ya muungano Narc.

Mwaka huo, vyama vya Ford Kenya, SDP na DP vilivyokuwa chini ya muungano wa NAK viliungana na LDP iliyokuwa ya waasi wa Kanu kisha kubuni muungano mkubwa wa Narc uliofanikiwa kushinda viti vingi bungeni.

Hata hivyo, itabidi Bw Odinga apige hesabu za kisiasa ili ODM ambayo imekuwa chama kikubwa zaidi nchini isalie na sifa hiyo hata baada ya muungano wa Azimio la Umoja kubuniwa.

Kwanza, wafuasi wa chama hicho watachanganyikiwa debeni iwapo ODM itasimamisha wawaniaji kwenye ngome yake ya kisiasa kisha pia kuwa na wagombeaji wa Azimio la Umoja.

Hali hii itayeyusha umaarufu wa chama hicho kwa kuwa iwapo Bw Odinga atatumia muungano mpya, basi wawaniaji wake ndio watakaopigiwa kura.

Aidha, hii itasababisha chama hicho kuwa hafifu na idadi ya sasa ya viti vya uwakilishi vinavyoshikiliwa na ODM itapungua sana baada ya kura za 2022.

Hali hii itanyima chama hicho cha upinzani mgao mkubwa wa kifedha kinaopata kutoka kwa hazina ya vyama vya kisiasa.

Kadhalika, kihistoria, baadhi ya vyama vilivyoishia kwenye muungano kuelekea uchaguzi mkuu hutokomea baada ya kura kufanyika, hali ambayo inaikodolea macho ODM.

Baada ya uchaguzi wa 2002, vyama vilivyokuwa ndani ya Narc mathalani DP, SDP Ford Kenya na LDP vilibakia vigae na kupoteza umaarufu wao.

Vivyo hivyo, vyama vilivyoingia ushirikiano na PNU kama KANU katika uchaguzi mkuu wa 2007 sasa havina usemi wao wa zamani mbali na kuwa na idadi ya chini mno ya madiwani, wabunge, maseneta na magavana.

Viongozi wa vyama vingi vilivyovunjwa kuelekea uchaguzi wa 2017 kisha kubuniwa kwa Jubilee, sasa wanajuta kufanya uamuzi huo, kwa sababu Jubilee yenyewe saa hii haina umaarufu hata katika zilizokuwa ngome yake ya kisiasa Mlima Kenya na Kati mwa nchi.

Hata baadhi ya waliovunja vyama vyao kama Naibu Rais Dkt William Ruto (URP), Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa (New Ford Kenya) na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi (APK) sasa wametoroka Jubilee kisha kubuni UDA, DAP-K na RBK mtawalia.

ODM imekuwa chama mahiri ambayo imepigania demokrasia na mageuzi tangu ibuniwe 2005 baada ya kampeni za marekebisho ya katiba ambayo mrengo wa ‘LA’ ulipata ushindi.

Kwa hivyo, haifai chama hiki kipotee hivi kutokana na kubuniwa kwa vuguvugu la Azimio la Umoja. Badala yake Bw Odinga ndiye anafaa kutumia tiketi ya chama hicho kuwania Urais jinsi ilivyokuwa katika muungano wa NASA 2017, kisha ODM itumike na wawaniaji mbalimbali kwa vyeo vya kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Waathiriwa wa moto kusubiri zaidi kujengewa makazi

CHARLES WASONGA: Wakulima wasaidiwe kunufaika kutokana na...

T L