• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 4:39 PM
Waathiriwa wa moto kusubiri zaidi kujengewa makazi

Waathiriwa wa moto kusubiri zaidi kujengewa makazi

Na SAMMY KIMATU

FAMILIA zaidi ya 100 ambazo nyumba zao ziliteketea mkesha wa Krismasi mwaka jana katika mtaa wa Kayaba, kaunti ndogo ya Starehe zitalazimika kusubiri zaidi kurudi makwao.

Hii ni baada ya wamiliki wa nyumba zilizoteketea kupanga kujenga nyumba za kudumu huku wengine wakisema hawatajenga upya kwa kukosa pesa.

Awali, nyumba hizo, katika eneo la Crescent zilikuwa zimejengwa kwa mabati jambo lililochangia moto kusambaa zaidi.

Tangu nyumba ziteketee wakati wenyeji walikuwa maeneo ya mashambani msimu wa sherehe, wakazi walipoteza mali ya thamani isiyojulikana.

Wakati huu, walioathirika wanaishi kwa marafiki, watu wa jamii zao na wengine kukaa kwa wasamaria wema wakisubiri kurudi makwao ama kuhamia kwingineko.

“Ni bora kujenga nyumba za mawe kuliko za mabati kwa kuwa za mawe zina uwezo wa kuzuia moto kuteketeza nyumba nyingi,” Bi Veronicah Njambi, mwathiriwa akanena.

Kufikia Jumanne, viongozi mbalimbali walitoa msaada kwa waathiriwa ili kuwapiga jeki wanapoanza maisha upya.

Vilevile, waathiriwa walipewa sufuria, magodoro, mitungi ya maji, sukari, mchele na unga huku wamiliki wa nyumba wakipata mabati kumi kila mmoja kutoka kwa wahisani.

Mkuu wa polisi katika eneo hilo, Bw Timon Odingo alisema polisi wanachunguza chanzo cha moto.

  • Tags

You can share this post!

Kitengo cha matibabu cha Uhuru Kenyatta Wing chazinduliwa...

CECIL ODONGO: Raila asiruhusu Azimio la Umoja limeze chama...

T L