• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
CHARLES WASONGA: Mbali na mlo serikali yafaa ikamilishe miradi Nyanza

CHARLES WASONGA: Mbali na mlo serikali yafaa ikamilishe miradi Nyanza

NA CHARLES WASONGA

ZIARA nyingi ambazo Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Bw Eliud Owalo amefanya kwa nia ya kusambaza chakula cha msaada katika kaunti za Luo Nyanza, zimefasiriwa kama zinazolenga kuwashawishi wakazi kuunga mkono Serikali ya Rais William Ruto.

Hii ni kwa sababu eneo hilo ni ngome ya kisiasa ya mpinzani mkuu wa Dkt Ruto, Bw Raila Odinga ambaye wakazi wamemuunga mkono kisiasa tangu 1997 alipowania urais kwa mara ya kwanza.

Katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, wakazi wengi wa kaunti za eneo hilo; Siaya, Migori, Homa Bay, na Kisumu, walimpigia kura Bw Odinga wakitumai kuwa angefaulu kuingia Ikulu katika jaribio lake la tano.

Lakini matokeo ya uchaguzi wa urais yalikwenda kinyume na matarajio ya wakazi hao na sasa Rais wa Kenya si Bw Odinga bali ni Dkt Ruto.

Kwa hivyo, ili wakazi wa eneo hilo wahisi kuwa sehemu ya taifa la Kenya linaloongozwa Serikali ya Kenya Kwanza, Bw Owalo amekuwa akiendesha kampeni ya kusambaza chakula cha msaada kwa wakazi walioathirika na makali ya njaa kufuatia ukame ulioshuhudiwa nchini kuanzia mwaka 2021.

Ninaunga mkono mpango unaoendeshwa na Waziri Owalo kwa niaba ya Rais Ruto ikizingatiwa kuwa katika miaka ya nawali ilikuwa nadra kwa wakazi wa maeneo haya kupokea chakula cha msaada kutoka kwa serikali.

Lakini kwa mtazamo wangu, hatua ya Bw Owalo, ambaye ni mzawa wa kipekee wa Luo Nyanza katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Dkt Ruto kusambaza chakula cha msaada kwa wakazi si suluhu ya kudumu kwa wakazi wa eneo hilo.

Kile ambacho Waziri Owalo, na wandani wa Rais Ruto kutoka eneo hilo wanafaa kufanya ni kuhakikisha serikali ya Kenya Kwanza inakamilisha miradi iliyoanzishwa na serikali iliyopita ambayo haijakamilishwa.

Miradi hiyo inayokadiriwa kugharimu Sh100 bilioni ni kama vile kuanzishwa kwa huduma za uchukuzi kutumia reli ya zamani kutoka Kisumu hadi Butere, kukamilishwa kwa makutano ya barabara ya Ahero (Ahero Interchange), mradi ulioanza 2017, na ujenzi wa bwawa la Koru-Soin unaotarajiwa kugharimu Sh25 bilioni.

Miradi mingine ni kukamilisha ujenzi wa barabara kuu ya Kisumu-Kakemega, ujenzi wa barabara ya pembeni kutoka Busia hadi Isebania kwa gharama ya Sh70 bilioni, upanuzi wa viwanja vidogo vya ndege vya Migori, Siaya, Suneka na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu, miongoni mwa miradi mingine.

Kwa sababu Rais Ruto aliahidi kukamilisha miradi yote iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, kabla ya kuanzisha miradi mipya, alenge kukamilisha miradi hii katika eneo la Nyanza.

Inatia moyo kwamba Rais anatarajiwa kuzuru Homa Bay hapo mwakani kuzindua mradi wa ujenzi wa nyumba 2,000 za makazi zenye gharama nafuu.

Mradi huo uliratibiwa na serikali iliyopita ya Jubilee kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Homa Bay.

Dkt Ruto pia anatarajiwa kuzindua ujenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Uvuvi cha Kabonyo katika eneo bunge la Kisumu Magharibi.

Ninaamini kuwa miradi kama hii ndiyo itakayochochea ukuaji wa kiuchumi wa eneo la Luo Nyanza na hivyo kuleta faida ya muda mrefu kwa wakazi.

Pamoja na usambazaji wa chakula cha msaada, utekelezaji wa miradi hii utawafanya wakazi kuchangamkia serikali ya Rais Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Museveni aondoa masharti makali ya kudhibiti tishio la Ebola

MAPISHI KIKWETU: Maini ya kukaanga kwa kitunguu saumu

T L