• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
CHARLES WASONGA: Ruto azingatie ahadi yake ya kutoangusha upinzani

CHARLES WASONGA: Ruto azingatie ahadi yake ya kutoangusha upinzani

NA CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya ushindi wake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuidhinishwa na Mahakama ya Upeo, Rais William Ruto alitangaza kuwa angependa mrengo wa upinzani wenye nguvu.

Upinzani ambao ungeangazia utendakazi wa serikali yake ili iweze kuwajibikia Wakenya waliomchagua kuwa rais wao.
Rais Ruto alisema ili kutimiza lengo hilo hangeteua viongozi wa upinzani (Azimio la Umoja- One Kenya) katika serikali yake au kuwashawishi kujiunga na Kenya Kwanza (KKA).

Lakini sasa inavunja moyo kwamba, Rais anaonekana kutenda kinyume na ahadi hiyo kwa kuanzisha kampeni ya kuwashawishi wabunge zaidi wa Azimio kujiunga na mrengo wa KKA.

Ni wazi kwamba, Dkt Ruto analenga kuhakikisha kuwa mrengo wake unapata uungwaji mkono wa angalau thuluthi mbili ya jumla ya wabunge katika bunge la kitaifa.

Ingawa hatua hii itawezesha KKA kupitisha miswada na hoja za kuiwezesha kutekeleza manifesto yake, kuna hofu kwamba inaweza kutumia mwanya huo kupitisha miswada yenye malengo ya kuendeleza utawala dhalimu nchini.

Mrengo wa KKA pia unaweza kutumia nafasi hiyo kudhamini miswada ya mageuzi ya katiba kwa ajili ya kuendeleza masilahi ya muungano huo, sawa na ule uliopendekezwa majuzi na Mbunge wa Fafi, Salah Yakub.

Japo Rais Ruto mwenyewe alijitokeza na kupuuzilia mbali pendekezo la Bw Yakub, la kuondolewa hitaji la kikatiba kwamba mtu ahudumu kama urais kwa mihula miwili pekee, matendo yake yanaashiria kinyume.

Naibu wake, Rigathi Gachagua na Naibu Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Owen Baya wamesema waziwazi mrengo wa KKA unalenga kuvutia wabunge 50 zaidi kutoka Azimio.

Juzi Rais Ruto mwenyewe alianza safari hiyo kwa kufanya mkutano, katika Ikulu ya Nairobi, na wabunge watatu kutoka kaunti ya Kakamega.

Baada ya mkutano huo, wabunge hao Emmanuel Wangwe (Navakholo), Benard Shinali (Ikolomani) na Titus Khamala (Lurambi), walisema “tutafanya kazi na Rais Ruto na serikali ili kuvutia miradi ya maendeleo kwa watu wetu.”

Duru zinasema kuna uwezekano mkubwa kwamba wabunge wengine kutoka eneo hilo watafuata nyayo za watatu hao.

Wakati huu, KKA ina jumla ya wabunge 179 baada ya wabunge wa vyama vilivyoko katika Azimio kujiunga na mrengo wa KKA baada ya Dkt Ruto kutawazwa mshindi.

Vyama hivyo ni kama vile United Democratic Movement (UDM), Maendeleo Chap Chap (MCC), Pamoja African Alliance (PAA) miongoni mwa vingine.

Ikiwa KKA itafaulu kushawishi wabunge 50 wa Azimio kuiunga mkono bungeni, upinzani utakuwa dhaifu zaidi kuliko ulivyo sasa, hali itakayoiwezesha serikali kupitisha miswada ya kufanyia marekebisho vifungu vya katiba vinavyohitaji uungwaji mkono kutoka angalau thuluthi mbili ya wabunge.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: GMO: Serikali ielimishe wananchi kuondoa dukuduku

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uhispania wabebesha Costa Rica...

T L