• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
DOUGLAS MUTUA: Mchokozi Putin aadhibiwe kwa Urusi kufukuzwa UN

DOUGLAS MUTUA: Mchokozi Putin aadhibiwe kwa Urusi kufukuzwa UN

NA DOUGLAS MUTUA

NINAZIDI kuamini kwamba, Umoja wa Mataifa (UN) unapasa kuvunjiliwa mbali na shirika jingine kubuniwa.

Kauli hii inatokana na maafa ya vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Vifo hivyo vinazidi kunisadikisha kuwa mataifa yanayodai kushikilia dunia kwa takriban kila kitu yameshindwa kuidhibiti.

La kushangaza, na vilevile kusikitisha ni kwamba, mataifa hayo tajiri na yenye uwezo mkubwa wa kijeshi yamekwama kutokana na kanuni zao wenyewe.

Kwamba, hayawezi kuwaokoa raia wa Ukraine wanaoangamizwa kama nzi na nduli Vladimir Putin, kisa na maana kanuni, ni fedheha kwao na dhihaka kwa thamani ya maisha ya binadamu.

Kwamba shirikisho la kijeshi la NATO haliwezi kuingilia kati, kisa na maana Ukraine si taifa mwanachama, ni ithibati kuwa dunia haina suluhu ya hatari zinazoikabili.

Umoja wa Mataifa bado unajikokota na kuwaza iwapo unapaswa kuwekea Urusi vikwazo vya kumlemaza Putin.

Sirejelei vikwazo vya kiuchumi, hivyo vimemwangukia Mrusi huyo kama makombora tangu aingie Ukraine siku 45 zilizopita.

Narejelea vikwazo vya kuifunga anga ya Ukraine isipae ndege hata moja kama vilivyowekewa marehemu Muammar Gaddafi wa Libya ili ang’olewe mamlakani.

Anga ikifungwa tu, itakuwa na maana kwamba ndege za kivita za Urusi haziwezi kuruka na kuangusha mabomu Ukraine kwa raha zao kama zinavyofanya sasa hivi.

Na zikithubutu zitakuwa zinavunja sheria za kimataifa, ambazo Marekani na mataifa mengine yenye nguvu na jukumu la kutetea na kulinda vikali.

Hatua hiyo itaipa nafasi Ukraine kuwafukuzia mbali wanajeshi wa Urusi wanaokabiliana nao upande wa mashariki.

Ikiwa majeshi ya Ukraine, yakiwa na silaha chache na zilizodhaniwa kuwa duni kuliko za Urusi, yamemkosesha Mrusi fahari ya kulitwaa jiji la Kyiv, unadhani yatamfanyiaje yakifungiwa anga?

Hii ya kufunga anga ni hisani ambayo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameiomba jamii ya kimataifa imfanyie ikiwa inataka Ukraine iishinde Urusi.

Lakini nina hakika jamii ya kimataifa haiwezi kufanya hivyo kwa kuwa hatua hiyo itaipa jukumu la kuikabili Urusi.

Mataifa yenye silaha za kiniuklia yanaepuka hali yoyote itakayoyaweka mkabala na Urusi katika vita vinavyoweza kuishia kuwa vikuu vya tatu vya dunia.

Mataifa yenye nguvu yaache mchezo, yaikomeshe Urusi mapema, ikibidi yaharibu uwezo wake wa kiniuklia kisha yaifukuze kutoka uanachama maalumu wa Umoja wa Mataifa unaoipa kura ya turufu, nafasi yake ipewe taifa la Afrika!

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Msisimko Mlima Kenya Spika Muturi akizungumza lugha ya...

Mtego wa Raila katika Azimio

T L