• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Msisimko Mlima Kenya Spika Muturi akizungumza lugha ya mahasla

Msisimko Mlima Kenya Spika Muturi akizungumza lugha ya mahasla

NA MWANGI MUIRURI

[email protected]

HATUA ya Spika wa bunge la kitaifa Justin Bedan Muturi ya kujiunga na mrengo wa uwaniaji urais wa Naibu wa Rais Dkt William Ruto imechambuliwa kuwa na msisimko aina yake katika Kaunti za Mlima Kenya.

Akiingia Kenya Kwanza Alliance na chama chake cha Democratic Party (DP), Bw Muturi alisema alichukua mkondo huo kutokana na shinikizo za wadau muhimu katika siasa za Mlima Kenya, wapigakura wakiwa nguzo kuu.

Alisema kuwa baada ya kupiga msasa mirengo yote iliyoko katika kivumbi cha Agosti 9, 2022, aliishia kufanya uamuzi kwamba Dkt Ruto ndiye yuko na sera na mwongozo mufti kwa taifa.

Alisema nia yake kuu katika tangazo lake la awali kuwa angewania urais ilikuwa ya kusaka maslahi ya kufaa watu wa Mlima Kenya na taifa lote kwa ujumla akiwa na mada ya kuunganisha wananchi ndani ya uzalendo, upendo na ustawi.

Alisema kuwa Dkt Ruto amewavutia viongozi wanaoonekana kuwa na ari isiyo na unafiki ya kuunganisha Wakenya.

“Niko katika jumuiya ya haki katika kuunganisha Wakenya tukiwa na Dkt Ruto, kinara wa Amani National Congress (ANC), Kinara wa Ford Kenya Bw Moses Wetang’ula na mwenzao wa Safina Jimi Wanjigi,” akasema Spika Muturi.

Kuna baadhi wanaosema kuwa mwelekeo huo wa Bw Muturi sasa unamweka pazuri kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto na hatimaye awe Naibu wa Rais ikiwa watashinda uchaguzi wa Agosti 9.

“Bw Muturi sio tu Spika bali ndiye wa pili kikatiba katika nguvu za serikali Mlima Kenya. Baada ya Rais Uhuru Kenyatta, Spika ndiye wa tatu katika mamlaka ya kikatiba, wa pili akiwa ni Naibu wa Rais,” akasema aliyekuwa afisa wa muda mrefu wa utawala Bw Joseph Kaguthi.

Bw Kaguthi alisema kuwa miaka 10 ya Bw Muturi akiwa Spika wa Bunge la Kitaifa inamweka pazuri kuwa na mtandao wa kitaifa ukiwa na mizizi katika maeneo bunge yote nchini na ambao unaweza ukamfaa kuwania urais katika siku za usoni.

Hata hivyo, umri hauko na Bw Muturi kwa kiwango kikuu kumwezesha kuwania urais katika chaguzi zijazo. Kwa sasa ako na miaka 65 na ambapo Dkt Ruto (iwapo atashinda urais) atahudumu kwa miaka 10, basi Bw Muturi katika Uchaguzi wa 2032 atakuwa na miaka 75.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Bw Harman Manyora alisema kwamba hatua ya Bw Muturi ya kujiunga na mrengo wa Dkt Ruto inaashiria kuwa nyanjani Mlima Kenya merikebu ya Azimio la Umoja-One Kenya Alliance haijavutia wenyeji.

“Hiyo Ina maana kuwa ushawishi wa Rais Kenyatta katika ngome ya Mt Kenya umedidimia. Wanasiasa wengi wa eneo hilo wanaoonekana kupendelea Dkt Ruto huku walio nyuma ya Rais wakionekana kususia kukumbatia uwaniaji wa Kinara wa ODM Bw Raila Odinga,” akasema.

Prof Manyora alisema kwamba umuhimu wa kura za Mt Kenya ni WA dhati katika ususi wa mbinu ya Ushindi na kwa sasa ikiwa Rais ataonekana kuzidi kuhepwa na kutengwa kunazua dhana kwamba wanaompigia debe Bw Odinga eneo hilo wako na kibarua kigumu.

Seneta wa Murang’a Dkt Irungu Kang’ata alisema kuwa ujio wa Bw Muturi ndani ya mrengo wa Dkt Ruto unatilia mkazo “ukweli kwamba kinara wa siasa za Mlimani kwa wakati huu ni Naibu wa Rais.”

Alisema kwamba hatua ya Bw Muturi ya kutangaza msimamo wake kwa sasa ndani ya Kenya Kwanza inaendeleza mpango unaoendeshwa kichinichini wa kuunganisha wapiga kura wa Mt Kenya.

“Tumekuwa tukilenga tuwe na Umoja wa watu wetu ndani ya mrengo mmoja. Hata Rais Kenyatta ambaye amekuwa jemedari sugu wa kutuelekeza kwingine nje ya merikebu ya Dkt Ruto tunamuomba tu arudi nyumbani,” akasema Dkt Kang’ata.

Ishara kuwa Bw Muturi alikuwa njiani kuingia mrengo wa Dkt Ruto zilianza kujitokeza mwanzoni mwa mwezi uliopita wakati binamuye Rais Kenyatta Bw Kung’u Muigai alisema kuwa uwaniaji wa urais wa Bw Odinga ulikuwa hatari kwa wapiga kura wa Mt Kenya.

Bw Muigai 72 ambaye pia ni mzee wa kijamii ndiye aliongoza hafla ya kumtawaza Bw Muturi kuwa msemaji wa Jamii za Mt Kenya, nafasi ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Rais Kenyatta.

Bw Muigai alisema kuwa barabara Rais Kenyatta anaongoza Watu wa Mt Kenya imejawa na hatari ya laana ambayo inafaa kutekelezewa tambiko ili iwe salama.

“Rais mwanzilishi wa taifa hayati Mzee Jomo Kenyatta(1963-1978) alipinga barabara hiyo vikali kiasi cha kuzindua hafla za ulishaji kiapo mwaka wa 1969.

“Mimi ndiye nilikuwa mmoja wa makatibu katika hafla hizo za kiapo katika eneo la Gatundu Kusini…Wanaojua kuhusu mila wanaelewa kwamba ili kubatilisha yaliyozimwa kupitia kiapo kwa njia iliyo salama huwa tu ni kupitia tambiko. Hilo halijafanyika na hadi sasa mkondo huo wa kisiasa ambao tunaelekezwa hautufai sisi ila tu, kwanza taambiko lifanywe likijumuisha wazee wa kijamii,” akaambia Taifa Leo.

Bw Muigai aliongeza kuwa hatua ya Rais ya kumusukuma kinara huyo wa ODM arithi urais baada ya Uchaguzi wa Agosti 9 haifai kuchukuliwa kama msimamo pana wa familia ya hayati Mzee Kenyatta.

Bw Muigai alisema kuwa kiapo hicho kilikuwa cha kuzima jamii ya Agikuyu kumkumbatia Mzee Jaramogi Oginga ambaye ni babake Bw Odinga kuibuka kuwa rais wa taifa hili. Alidai kuwa kiapo hicho pia kililenga wandani wa Bw Oginga.

Aidha alisema kuwa kuna mengine mengi kuhusu Bw Oginga ambayo yalijumuishwa katika kiapo hicho na ambapo kwa ujumla yanageuza uwaniaji wa Bw Odinga kuwa unaohitaji kwanza kuandaliwa tambiko kabla ya kukubalika na kufuatwa katika eneo la kati.

Bw Kaguthi alisema kuwa ni ukweli kiapo hicho kilitekelezwa katika maeneo mengi ya kati.

“Masuala ya kiapo na tambiko yakiangaziwa kwa macho ya mila huwa ni nyeti. Lakini tukiingiza siasa mambo hugeuka na kuanza kuonekana kama kuna utundu. Lakini kile kilichoko wazi ni kwamba, yaliyokatazwa kupitia kiapo ni lazima yaandaliwe tambiko ili yakubalike. Mzee Muigai ako na hoja nyeti lakini sitaki kujiingiza katika mjadala huo katika mada ya kiapo, siasa na watu binafsi hasa katika msimu huu wa kisiasa,” akasema.

Bw Muigai alipuuzilia mbali hoja kwamba anaangazia familia ya Kenyatta kama isiyo na uwiano kuhusu msimamo wa kisiasa.

“Sio mara ya kwanza ambapo familia yetu inatofautiana kuhusu mkondo wa kisiasa. Itakumbukwa kwamba mwaka wa 2002 Bw Kenyatta aliwania urais akiwa na chama cha Kanu lakini dadangu mkubwa Bi Beth Mugo akawania kiti cha ubunge cha Dagoretti Kusini kwa muungano wa Narc ukimfadhili Mwai Kibaki kuwa rais,” akasema. Bi Mugo ni Seneta maalum ambaye kwa sasa ako na miaka 82.

Bw Muigai alisema kuwa wazee wako tayari kushirikisha tambiko hilo ili kufanya uwaniaji na kukubalika kwa Bw Odinga.

“Nikiangalia matukio ambayo yanafanyika katika jamii yetu ya Agikuyu ninasikitika si haba. Tumegawanya na kutawanywa kiasi kwamba tunachukiana kwa misingi duni ya kupigia debe wasio wa jamii yetu. Tumegawanyika tukipigia debe wawaniaji wa jamii zingine. Tunafaa rurejelee umoja wetu na tupige kura kwa kapu moja ili wingi wetu utufae katika mgao wa keki ya kitaifa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mvurya ampigia naibu wake debe

DOUGLAS MUTUA: Mchokozi Putin aadhibiwe kwa Urusi kufukuzwa...

T L