• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Mtego wa Raila katika Azimio

Mtego wa Raila katika Azimio

NA LEONARD ONYANGO

VIONGOZI wa zaidi ya vyama 20 vilivyo katika Azimio la Umoja-One Kenya wamefungwa ndani ya muungano huo na hawataruhusiwa kujiondoa hadi Machi 2023.

Kulingana na mkataba ambao umewasilishwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu, hakuna chama kitaruhusiwa kujiondoa kutoka kwenye muungano huo miezi sita kabla na miezi mitatu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Kifungu hicho kinalenga kumkinga Bw Odinga dhidi ya kuhangaishwa na wanasiasa wanaotishia kujiondoa kwenye muungano mara kwa mara.

Aidha, kinalenga kumpa Bw Odinga fursa ya kuunda serikali bila vitisho kutoka kwa washirika wa muungano huo.

Mkataba huo ulitiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta, Bw Odinga na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Rais Kenyatta anawakilisha vyama 15 vilivyo chini ya mwavuli wa Jubilee huku Bw Kalonzo akitia saini kwa niaba ya vyama vilivyo katika muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Kulingana na mkataba ambao Taifa Leo imeona, chama kinachotaka kujiondoa miezi mitatu baada ya Agosti 9, ni sharti kiandike ilani ya siku 90.

Barua ya kujiondoa itatumwa kwa Baraza Kuu la Azimio la Umoja-Kenya Kwanza ambapo itajadiliwa na kisha kuto uamuzi.

“Hakuna chama kitaruhusiwa kujiondoa kutoka kwenye muungano miezi sita kabla ya Agosti 2022 au miezi mitatu baada ya Uchaguzi Mkuu,” unasema mkataba huo.

Hiyo inamaanisha kuwa kuanzia kesho Bw Odinga atapata afueni kwani hatakuwa akihangaishwa na wanasiasa wanaotaka kujitoa.

Leo ilikuwa siku ya mwisho kwa vyama kujiunga na miungano ya kisiasa, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Kisiasa iliyotiwa saini na Rais Kenyatta Januari 2022.

Jumatano, Bw Odinga alipigwa na butwaa baada ya viongozi wa vuguvugu linalojiita Mwanzo Mpya linloongozwa na Gavana wa Machakos kutishia kujiondoa katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Viongozi hao walilalamikia ‘kufinywa’ ndani ya muungano wa Azimio tangu Bw Musyoka kutangaza kuunga mkono Bw Odinga.

Viongozi hao walitaka chama cha Wiper kisiachiwe kusimamisha wawaniaji katika eneo la Ukambani. Vilevile, walitaka mwaniaji mwenza wa Bw Odinga ateuliwe na wajumbe wa vyama vilivyo ndani ya muungano wa Azimio.

“Masula yaliyo ndani ya mkataba wa muungano hatujayaona hivyo tunataka utolewe kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa tutie saini yetu ndipo urudishwe,” wakadai viongozi hao wa vuguvugu la Mwanzo Mpya linalojumuisha vyama vinane kama vile DAP-K kinachoongozwa na Waziri wa Usalama Eugene Wamalwa, Narc chake Gavana wa Kitui Charity Ngilu na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana kati ya wengineo.

Baada ya kutishia kujiondoa, Dkt Mutua Alhamisi alidai kwamba alipokea simu kutoka kwa Naibu wa Rais William Ruto akimtaka kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza.

Madai hayo ya Gavana Mutua yalionekana kumshtua Bw Odinga ambaye alikimbia mara moja na kuandaa mkutano na viongozi wa Mwanzo Mpya Alhamisi.

Katika mkutano huo, Bw Odinga alikubali matakwa ya kutaka mwaniaji mwenza wake ateuliwe na wajumbe na kila chama kiruhusiwe kusimamisha wawaniaji kote nchini bila kizuizi.

Maafikiano hayo, hata hivyo, yamezua tumbojoto katika kambi ya Bw Musyoka ambaye jana alifanya kikao na mawakili wa OKA.

Bw Musyoka jana Ijumaa alitishia kujiondoa Azimio la Umoja-One Kenya huku akitaka kuonyeshwa makubaliano ya kisiri yaliyofanywa baina ya Bw Odinga na viongozi wa Mwanzo Mpya.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Mchokozi Putin aadhibiwe kwa Urusi kufukuzwa...

Leicester na PSV waumiza nyasi bure katika mkondo wa kwanza...

T L