• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
DOUGLAS MUTUA: Tusisukume wanariadha wetu kusaka uraia wa nchi za kigeni

DOUGLAS MUTUA: Tusisukume wanariadha wetu kusaka uraia wa nchi za kigeni

NA DOUGLAS MUTUA

HIVI Wakenya tumeingiza saratani yetu ya ufisadi kwenye michezo ya riadha, au wanariadha wetu wamekuwa wazembe?

Mojawapo ya kauli za kuvunja moyo nilizosikia nikiwa shuleni ni kwamba, mchezo wa kandanda nchini ulijaa mapendeleo na ufisadi.

Wengi walikariri kwamba, ili uruhusiwe kucheza mpira, hasa katika timu ya taifa – Harambee Stars – sharti uwe unajulikana au upeane hongo nono.

Ithibati ya uozo kwenye kandanda ilionekana pale kocha maarufu, marehemu Reinhardt Fabisch, alipoteuliwa mkufunzi wa timu ya taifa katikati ya miaka ya tisini.

Aliivunjilia mbali Harambee Stars tuliyozoea, akasazwa beki Musa Otieno pekee, vijana machachari wakasajiliwa kutoka klabu zisizojulikana, Kenya ikaanza kuinuka.

Wasemao husema mazoea yana taabu; Fabisch hakudumu muda mrefu kabla ya bughudha za fatani Wakenya kumuandana, akaondoka, nayo kandanda ikazama tena.

Matatizo ya kandanda hayo; riadha ina yake pia: ufisadi, maandalizi duni, matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku, wanariadha kutozwa ushuru mara mbili wakishiriki mashindano ya kimataifa na kadhalika.

Kwa jumla, ukiwa mwanamichezo nchini Kenya, wewe ama ni kitega uchumi cha wazembe wasiokata jasho, au huheshimiwi na yeyote. Unazoeleka.

Kwa kuwa wanamichezo si wabishi, ukandamizaji dhidi yao unaweza kuendelea mfululizo.

Kawaida yao hufa kikondoo, hawalalamiki dhidi ya kupe wanaodandia safari zao wanapokwenda kushiriki mashindano ya kimataifa nje ya nchi.

Jiulize ni vipawa vingapi ambavyo vitadumazwa na mtindo huu, vijana ambao wangefaulu maishani waponzeke na kubaki vijijini wakilewa.

Mjinga naye tangu hapo akierevuka, mwerevu huwa mashakani.

Wanariadha wetu wameanza kuchukua uraia wa nchi nyingine kimya-kimya.

Hawajaanza juzi, lakini idadi ya wazawa – tena wazuri tu – wanaowakilisha mataifa mengine katika mashindano ya kimataifa inatia hofu.

Nacho kiwango chetu cha ushindani kwenye mbio kinazidi kushuka kila mwaka, sasa Kenya si mfalme wa riadha tena.

Tunatishiwa hata na Wazungu huku damu yetu ikitumikia mataifa mengine kwa sababu hatujaithamini inavyotakikana.

Waliojanjaruka na kupata fursa za kujiendeleza nje ya Kenya wanawika katika mashindano ya dunia ya riadha yanayoendelea Amerika.

Hebu na tuache kuwabeza wanariadha wetu, tuwahudumie na kuwasaidia kwa vyovyote vile, ikiwa hatutaki kupoteza au kugawana fahari ya ushindi na mataifa yanayowathamini na kuwapa uraia.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Vipusa wa Uswidi kuvaana na Uingereza kwenye nusu-fainali...

Babu kortini akidai kuwa mwanawe Rais Kibaki

T L