• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
WANDERI KAMAU: Hadhi ya usomi isidunishwe kwa kutoa vyeti kwa wasiojua safari halisi

WANDERI KAMAU: Hadhi ya usomi isidunishwe kwa kutoa vyeti kwa wasiojua safari halisi

Na WANDERI KAMAU

MASOMO ni kama kazi yoyote ile yenye uchovu.

Si rahisi hata kidogo.

Ni sababu hiyo ambapo baada ya muda fulani, wanafunzi hupewa muda na walimu wao kwenda kupumzika kidogo halafu kurudi shuleni baadaye.

Walimu vile vile hupata muda wa kupumzika, kutathmini yale waliyowafunza wanafunzi na mikakati watakayoweka kuhakikisha watamaliza silibasi na kupita mitihani yao. Bali na kuwa kazi, elimu pia ni safari. Safari ya nyikani, miinuko na mabonde.

Ni safari yenye pandashuka nyingi, ambapo mwanafunzi hulazimika kuwa na uvumilivu mwingi ili kuhimili changamoto hizo.

Pengine wale wanaoweza kueleza juhudi ambazo mtu huweka ili kufanikiwa masomoni ni maprofesa au madaktari waliofanikiwa kusoma hadi katika kiwango cha shahada ya uzamifu.

Ni safari ambayo humlazimu mtu kuzama vitabuni, kujinyima raha au hata wakati mwingine kukosana na jamaa na marafiki.

Hata hivyo, mwishowe huwa ni mafanikio makubwa maishani.Licha ya hayo yote, inasikitisha kuona baadhi ya watu wenye tamaa wakipitia njia za mkato kupata utambulisho wa ‘Daktari’ ama ‘Profesa’ bila kupitia utaratibu unaofaa.

Uovu huu umefanikishwa na mchipuko wa taasisi za kila aina, zinazodai “kuwatambua watu waliotoa michango muhimu katika ustawi wa jamii.”

Kwanza, nyingi za taasisi hizo ni za kigeni, ambapo hata hazina kibali chochote kuendesha shughuli za masomo kutoka kwa Tume ya Elimu ya Juu (CUE).

Nyingi pia zinasimamiwa na mashirika yaliyosajiliwa ng’ambo.

Hivyo, uhalisia uliopo ni kuwa mengi ya mashirika hayo hata hayana ufahamu kuhusu utaratbu maalum kuhusu elimu ya juu nchini.

Katika hali hiyo, wakati umefika kwa tume hiyo kuanza msako mkali dhidi ya taasisi zote ambazo zinadai kutoa shahada za uzamifu “kuwatuza watu walioisaidia jamii.”

Kwanza, ni taratibu zipi zinazofuatwa katika kutoa shahada hizo? Kuna taratibu za kuwapiga msasa wanaopendekezwa kupewa shahada hizo?

Je, taasisi hizo zimefikisha viwango vya elimu ya juu kama inavyohitajika kisheria?Katika siku za hivi karibuni, imekuwa kawaida kumsikia karibu kila mtu maarufu akidai kuwa “Daktari.”

Naam, ‘daktari’, aliyetuzwa shahada ya uzamifu kwa “mchango” wake kwa jamii.

Mtindo huu umekolea sana miongoni mwa viongozi wa kidini, ambapo baadhi yao hata huwa wanakumbwa na ugumu kujieleza kwa lugha za kawaida kama Kiswahili au Kiingereza!

Kando na hayo, mafundisho ya wengine wao yamekuwa yakitiliwa shaka, kwani fasiri zake ni upotoshaji wa wazi kwa jamii.

Je, tunaishi katika nyakati zipi, ikiwa watu kama hao ndio wanakwezwa kutambuliwa na jamii kuwa ‘madaktari’ na ‘maprofesa’? Ni lazima taasisi kama CUE ziwajibike.

Hatuwezi kuishi katika mazingira ambapo watu ambao hawajapitia utaratibu ufaao wa kimasomo hujikweza bila kufuata njia zifaazo.

Hatuwezi kuishi katika hali ambapo kila mtu tajiri anakwezwa na taasisi yoyote ile kuwa ‘daktari’ ama ‘profesa’ ilhali kuna madaktari na maprofesa waliosoma na kutoa michango ya kweli kwa ustawi wa jamii.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Msichague ‘maadui’ wa serikali – Kibicho

Raila aahidi kuigeuza Lamu iwe ‘Dubai ya Afrika’

T L