• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Msichague ‘maadui’ wa serikali – Kibicho

Msichague ‘maadui’ wa serikali – Kibicho

Na WAWERU WAIRIMU

KATIBU wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho, amewarai Wakenya kuwachagua viongozi wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Kibicho alisema hiyo ndiyo njia pekee itakayohakikisha wamepata maendeleo.

Alisema viongozi hao watawaletea maendeleo makubwa ikilinganishwa na wale wanaoendelea kuikosoa serikali.

“Ni viongozi wanaoiunga mkono serikali pekee watakaohakikisha shule nyingi zimejengwa, raia wamepata maji na barabara zimewekwa lami baada ya Rais Kenyatta kung’atuka uongozini,” akasema Dkt Kibicho.

Alisema hayo alipoongoza hafla ya kuchangisha pesa kusaidia katika ujenzi wa bweni katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Merti, Kaunti ya Isiolo.

Katibu huyo alikuwa ameandamana Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) Wambui Nyutu na Bi Tiya Galgalo, aliye kamishna katika Tume ya Kitaifa kuhusu Ardhi (NLC).

Hafla hiyo ilikuwa imepangwa na Naibu Waziri wa Elimu, Mumina Bonaya.

Katibu huyo pia aliwarai Wakenya kufuata mwelekeo wa kisiasa watakaopewa na Rais Kenyatta, uchaguzi huo unapoendelea kukaribia.

Dkt Kibicho alisema nia ya Rais ni kuona Kenya imepata ustawi katika nyanja zote. Alieleza kwamba kila mmoja anayemuunga mkono Rais Kenyatta ni rafiki yake.

“Kuweni tayari. Mwelekeo atakaotupa Rais Kenyatta ndio tutakaofuata,” akasema, alipowahutubia mamia ya wenyeji waliofika katika hafla hiyo.

Katibu pia alitoa hakikisho kwa wenyeji kwamba serikali itarahisisha utaratibu wa wenyeji kuchukua vitambulisho vya kitaifa.Alisema hilo litawasaidia vijana katika eneo la Kaskazini Mashariki kutafuta nafasi za kazi.

“Serikali itawawezesha vijana katika eneo hili kupata vitambulisho kwa urahisi ili kuhakikisha wamefaidika kwa huduma inazotoa. Hilo pia litawasaidia kujiepusha na matumizi ya mihadarati,” akasema.

Katibu alitoa msaada wa magunia 100 ya mchele na mengine 200 ya maharagwe kwa familia zilizoathiriwa na njaa katika Kaunti Ndogo ya Merti.

Baadaye, alizindua ujenzi wa afisi ya elimu katika eneo hilo.

Ujenzi wa afisi hiyo unatarajiwa kuwarahisishia mzigo maafisa wa elimu katika eneo hilo wa kukodisha afisi.

Ujenzi wake unafadhiliwa na Wizara ya Elimu.

Ujenzi huo umepangiwa kumalizika katika muda wa miezi miwili.

Vile vile, Katibu alitangaza mpango wa serikali kubuni Kaunti Ndogo ya Cherab ili kuboresha huduma za serikali kwa wenyeji na kuimarisha hali ya usalama.

“Ningetaka kutangaza mpango wa serikali kubuni Kaunti Ndogo mpya. Hili ni kutokana na ombi ambalo limewasilishwa na Bi Bonaya,” akasema.

Bi Galgalo aliwarai wenyeji kumuunga mkono Bi Bonaya, ambaye ameeleza nia ya kuwania nafasi ya Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo mwaka 2022.

Vile vile, aliliomba Baraza la Wazee la Jamii ya Waborana kumuunga mkono kwenye azma yake.

You can share this post!

Mfanyabiashara kufungwa kwa kubomoa kanisa

WANDERI KAMAU: Hadhi ya usomi isidunishwe kwa kutoa vyeti...

T L