• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Hotuba ya Uhuru ichochee kuondoa ubaguzi na dhuluma

TAHARIRI: Hotuba ya Uhuru ichochee kuondoa ubaguzi na dhuluma

Na MHARIRI

RAIS Uhuru Kenyatta alitoa hotuba ya Jamhuri Dei jana Jumapili ambayo wapenzi wa historia bila shaka wataiona kuwa ya kusisimua.

Ilikuwa hotuba iliyosheheni historia ndefu ya taifa letu kuanzia enzi za ukoloni na juhudi za upiganiaji uhuru hadi pale ambapo nchi ya Kenya iliweza kuwa jamhuri.

Rais alieleza kwa kirefu kiini cha kukongamana katika Bustani ya Uhuru, akisema jinsi eneo hilo ndiko bendera ya Mkoloni iliteremshwa na ya Kenya ikapandishwa katika kilele cha Mlima Kenya.

Alisema hayo akielezea jinsi serikali inavyojenga makavazi ya kitaifa katika bustani hiyo ili kuhifadhi historia na matukio yote yaliyochangia ukuaji wa nchi hii, mazuri na mabaya.

Kuanzia juhudi za mashujaa waliokomboa nchi mpaka tukio lililotikisa taifa hili, la ghasia za 2008 hadi kwa mpango wa maridhiano ya kitaifa almaarufu BBI uliofanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 uliozua ubishi kati yake na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bw Kenyatta alisema taifa lilipoteza takriban Sh1 trilioni kutokana na msukosuko uliotokana na uchaguzi huo uliozua ubishi.

Kimsingi hotuba hiyo ilionyesha jinsi dhuluma na ubaguzi kwa njia moja au nyingine vilikuwa donda sugu tangu zamani.

Na hapa ndipo tatizo lilipo. Madhila haya mawili bado ni donda sugu leo.

Kila mahali unapotazama, unaona jinsi taswira ya “wenye nchi”na wananchi inavyojitokeza.

Unakuta mtu mmoja ana mali aliyojilimbikizia na akiwa mbioni kujipatia hata zaidi huku maelfu ya wengine hawana chochote, hata kupata mlo mmoja wa siku ni tatizo.

Na la kusikitisha zaidi, mali aliyojilimbikiza imetokana na kukata kona na ubadhirifu wa pesa za umma ambazo zingelitekeleza miradi ambayo inafaidi wengi moja kwa moja.

Serikali inatenga pesa kwa vikundi mbalimbali vya vijana, kina mama na walemavu, lakini kunatokea mtu anachota karibu robo tatu ya pesa hizo na kutoweka, na kuacha wengi ambao walikuwa wafaidi kwa kupata mtaji wa kuanzisha biashara ndogondogo wakibaki hoi.

Na la mno zaidi, wale waliojilimbikizia mali na waliofanya hivyo kwa pupa isiyomithilika wanaanza kutumia hela hizo hizo kuhonga wapigakura ili kuchaguliwa katika viti mbali mbali ambavyo wanatumia nyadhifa hizo kulinda mali zao na kusambaratisha kesi endapo wanaposhtakiwa.

Miaka 58 ya jamhuri na tuwe watu wenye utu.

You can share this post!

Ndoto ya BBI lazima itatimizwa, Uhuru asema

ELIMU MSINGI: Binti mfumaji mazulia

T L