• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
KAMAU: Kiboko kirejee shuleni ili kuboresha nidhamu

KAMAU: Kiboko kirejee shuleni ili kuboresha nidhamu

Na WANDERI KAMAU

TUNAISHI katika nyakati ngumu sana.

Nyakati za mahangaiko na wasiwasi.

Ni nyakati ambazo wazazi wanaishi kwa hofu na mashaka kuhusu usalama na mustakabali wa kimaadili wa watoto wao.

Malezi ya watoto wa kizazi cha sasa yamegeuka kuwa kibarua kigumu ambacho kinaonekana kuwashinda wazazi wengi.

Kinyume na awali, mazingira ya sasa ni magumu na yenye majaribu mengi. Wazazi wanazungukwa na kila aina ya maovu.

Ni kama mtu aliye katikati ya moto mkubwa akijaribu kujinusuru ili asichomeke.

Urejeleo huu unatokana na msururu wa visa vya utovu wa nidhamu shuleni, hasa miongoni mwa wanafunzi walio katika shule za upili.

Kila kunapokucha, hukosi kusikia kisa kuhusu mwanafunzi aliyetoroka shuleni, mwingine aliyempiga au kumtukana mwalimu au wanafunzi waliogoma baada ya kuchoma shule zao.

Mwezi uliopita, mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Gathiru-ini, Kaunti ya Kiambu, aliuawa katika hali tatanishi, baada ya kupatikana usiku katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Komothai, kaunti iyo hiyo.

Ingawa bado uchunguzi unaendelea kubaini jinsi mvulana huyo na wenzake walivyofaulu kuingia katika shule hiyo, kisa hicho kilidhihirisha utepetevu wa kinidhamu ulio katika shule za mabweni nchini.

Kulingana na ripoti kadhaa za uchunguzi kuhusu hali ya nidhamu katika shule hizo, imebainika imekuwa kawaida kwa wavulana kutoroka shule zao na kwenda katika shule za wasichana.

Imebainika kuwa njama hizo huwa ni mpango wa baadhi ya wavulana na wasichana ambao ni “wapenzi.”

Mara nyingi, mipango hiyo hufaulu kutokana na uwepo wa simu.

Baadhi ya shule huwa hazina sheria kali kuwazuia wanafunzi kuingia kwa simu wanaporejea kutoka likizoni, hali ambayo imekuwa ikiwawezesha kufanya kila aina ya maovu wakiwa ndani ya shule zao bila ufahamu wa walimu na wasimamizi wakuu.

Kutokana na kurahisika kwa njia za mawasiliano, wanafunzi hao pia wamekuwa wakidaiwa kuwahonga baadhi ya walimu na walinzi wa shule zao.

Hilo huwapa uhuru kufanya lolote watakalo bila kuogopa kuchukuliwa hatua yoyote.

Utepetevu uo huo wa kinidhamu ndio unatajwa kuchangia ongezeko la migomo na visa vya wanafunzi kuchoma mabweni yao.

Kufikia sasa, zaidi ya shule 20 zimefungwa kote nchini baada ya kuchomwa au wanafunzi kugoma.

Cha kushangaza ni kuwa, visa hivi ni mtindo ambao umekuwa ukishuhudiwa kila mwaka, hasa mitihani ya kitaifa inapokaribia.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Wizara ya Elimu mapema mwaka huu, mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) imepangiwa kufanyika Machi 2022.

Hivyo, wanafunzi wengi wanaripotiwa “kuiogopa” mitihani hiyo, hasa baada ya kukaa nyumbani kwa karibu mwaka mmoja kutokana na janga la virusi vya corona.

Bila shaka, imefikia wakati utepetevu huu wa kinidhamu ukome.

Ni lazima wazazi, walimu na wadau wote katika sekta ya elimu kuwajibika kuwaadhibu vilivyo wanafunzi wanaowapotosha wenzao.

Ni wakati viboko virejeshwe shuleni kama ilivyokuwa awali ili kulainisha kizazi hiki kinidhamu.

La sivyo, tutajilaumu wenyewe katika siku za baadaye.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Hofu kaunti 22 kuacha deni la mabilioni ya miradi hewa...

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa waovu hutumia njia za...

T L