• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Hofu kaunti 22 kuacha deni la mabilioni ya miradi hewa – ripoti

Hofu kaunti 22 kuacha deni la mabilioni ya miradi hewa – ripoti

Na LEONARD ONYANGO

MAGAVANA 22 wanaohudumu muhula wa pili, wataachia raia na warithi wao mzigo mzito wa madeni hewa ya mabilioni ya fedha watakapokamilisha muda wao mwaka 2022.

Ripoti ya Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) iliyotolewa Jumanne, inaonyesha kuwa serikali za kaunti zinadaiwa jumla ya Sh31.6 bilioni na wakandarasi hewa kufikia Juni 30, 2021.

Hali hii, inamaanisha kwamba hakuna ushahidi wa kuridhisha wa kuthibitisha kuwa wanakandarasi hao walitoa huduma au bidhaa kwa serikali za kaunti husika.

Magavana wa muhula wa pili watakaoacha mzigo mkubwa wa madeni yanayotiliwa shaka ni kiongozi wa Mombasa Hassan Joho (Sh 1.8 bilioni), Salim Mvurya (Kwale, Sh1.6 bilioni), Cyprian Awiti (Homa Bay, Sh1.4 bilioni) na Josphat Nanok (Turkana) Sh1.1 bilioni).

Wengine ni magavana Martin Wambora (Embu), Sh878 milioni, Paul Chepkwony (Kericho) Sh462 milioni), Patrick Khaemba (Trans Nzoia) Sh414 milioni) na Alfred Mutua (Machakos) Sh344 milioni), Amason Kingi (Kilifi) Sh245 milioni, James Ongwae (Kisii), Sh214 milioni na Ali Roba (Mandera) Sh203 milioni kati ya wengineo.

Magavana wa muhula wa pili walio na kiasi cha chini zaidi cha madeni ya wanakandarasi wanaotiliwa shaka ni Prof Kivutha Kibwana (Makueni, Sh2 milioni), Wycliffe Oparanya (Kakamega, Sh3 milioni).

“Suala la kuwepo kwa kandarasi zinazotiliwa shaka ni changamoto kubwa kwani hiyo ni ishara ya matumizi mabaya ya fedha za umma,” inasema ripoti ya CRA.

Mwenyekiti wake, Dkt Jane Kiringai, sasa anataka Bunge, Hazina Kuu ya Kitaifa na Ofisi ya Mdhibiti wa Bajeti, kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa kandarasi zinatolewa kwa uwazi kuzuia kupotea kwa fedha za umma.

Dkt Kiringai anasema kuwa uongozi wa serikali za kaunti unapobadilika bila kulipa kandarasi zinazotiliwa shaka, huwa changamoto kubwa kwa gavana mpya anayechukua hatamu za uongozi.

Kwa mujibu wa ripoti, magavana wapya wa Nairobi, Nakuru, Pokot Magharibi, Laikipia, Vihiga, Kitui, Nyandarua, Tana River, Kirinyaga na Kisumu walirithi kutoka kwa watangulizi wao kiasi cha juu cha madeni ya wakandarasi hewa kutoka kwa watangulizi wao baada ya uchaguzi wa 2017.

Nairobi inaongoza kwa kuwa na deni kubwa zaidi lililotokana na kandarasi ambazo zimetiliwa shaka. Nairobi inadaiwa Sh11.2 bilioni, Nakuru (Sh 2 bilioni), Pokot Magharibi (Sh 1.2 bilioni), Laikipia (Sh912 milioni), Vihiga (Sh730 milioni), Kitui (Sh567 milioni), Kirinyaga (Sh545 milioni), Nyandarua (Sh 524 milioni), Tana River (Sh696 milioni) na Kisumu (Sh604 milioni).

Kulingana na Dkt Kiringai, wengi wa magavana waliochaguliwa 2017, wamekataa kulipa madeni hayo yanayotiliwa shaka.

“Vilevile, warithi wa magavana watakaokamilisha muhula wa pili mwaka ujao, huenda wakakataa kulipa madeni hayo yanayotiliwa shaka,” akasema.

Wakati huo huo, Nairobi inaongoza kwa kuwa na kiasi kikubwa cha madeni ambayo yamethibitishwa kuwa halali.

Nairobi inadaiwa jumla ya Sh6.6 bilioni ikifuatiwa na Nakuru (Sh2 bilioni), Mombasa (Sh1.8 bilioni), Isiolo (Sh567 milioni) na Vihiga Sh422 milioni.

Kaunti zilizo na kiasi cha chini cha madeni yaliyothibitishwa kuwa halali ni Busia (Sh1 milioni), Kisumu (Sh4 milioni) na Trans Nzoia (Sh7 milioni).

You can share this post!

Seneta Ledama Olekina kuwasilisha kesi mahakamani kupinga...

KAMAU: Kiboko kirejee shuleni ili kuboresha nidhamu

T L