• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa waovu hutumia njia za mkato kushinda kura

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa waovu hutumia njia za mkato kushinda kura

Na KINYUA BIN KINGORI

HUENDA Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikakosa kutimiza shabaha yake kutokana na idadi ndogo ya raia waliojitokeza kusajiliwa.

IEBC ilikuwa imelenga kusajili Wakenya zaidi ya milioni sita wakiwemo vijana ambao wamechukua vitambulisho baada ya kutimiza umri wa miaka 18.

Kulingana na takwimu za Tume, kipindi hiki ndicho imesajili idadi ndogo zaidi ya wapigakura; kinyume na ilivyotarajiwa kutokana kwamba uchaguzi mkuu umekaribia.

Wengi watalaumu IEBC kwa kuzembea katika wajibu wake wa kutoa elimu ya kuwapa hamasisho wananchi, hasa vijana, kuelewa umuhimu wa kusijasili kama wapiga kura.

Kuna pia kundi la pili, ambalo limesuta wanasiasa kwa kutumia muda mwingi kupiga siasa za Azimio la Umoja, Hustler Nation na OKA; badala ya kuibuka na mbinu tamanifu na zenye kuvutia vijana wajisajili kupiga kura Agosti 9, 2022.

Wakenya wengi hawana hamu tena na siasa za upigaji wa kura baada ya matumaini yao kufifishwa na viongozi waliofeli kutimiza ahadi chungu nzima za mwanzoni.

Hata hivyo, mikakati bora ambayo imewekwa na tume ya IEBC itazima tabia ya wanasiasa kusafirisha watu kutoka mbali ili wajisajili kuwa wapiga kura katika maeneo ambako viongozi hao wanawania viti mbalimbali, kwa hongo.

Wanasiasa kwa muda mrefu wakati wa usajili humwaga pesa ili ‘kununua’ hizi kura za nje kufanikisha mpango wa kuchaguliwa kwao.

Pengine kuzimwa kwa mbinu hii chafu ndiko kulichangia idadi ndogo ya usajili wa wapiga kura kipindi hiki; maana wanasiasa wengi waliogopa kunaswa wakiendeleza ukora huu.

Ili mtu kukubaliwa kuhamisha kura yake kutoka eneo moja hadi lingine wakati huu, alihitaji barua ya chifu kuthibitisha ni mkaazi wa eneo hilo.

Ni kanuni hii ambayo ilichangia pakubwa idadi ndogo ya usajili kwani ilipangua njama hii fiche inayopendwa na wanasiasa wazembe kuchaguliwa.

Majuzi, mwanasiasa mmoja kutoka Garissa alihusishwa na njama ya kununua watu 100 walionaswa wakisafirishwa kutoka Kilifi.

Ukora huu umekuwa ukiendelezwa katika maeneo mbalimbali, ndiposa wakati mwingine viongozi wabaya wasio na sera wala maono huishia kuchaguliwa; matokeo ambayo hufanya wakaazi kubaki wameshika tama wasijue kiongozi huyo asiyefaa alichaguliwa na nani, kiasi cha kuhisi kwamba kura ziliibwa.

Kumbe wapigakura wengi waliomchagua walikuwa wamesafirishwa ili kumpigia kura mwanasiasa husika.

Ndiposa inakuwa vigumu kwa kiongozi kama huyo kuwahudumia wakazi ipasavyo ili kuimarisha maisha yao, sababu waliomchagua ni wageni walioletwa hapo kwa hongo tu.

Tume ya IEBC pia ibuni mbinu zaidi za kuhakikisha hongo katika uchaguzi inadidimia kabisa.

Ni wanasiasa tu waovu, wabaya na wasiojiamini ndio hutumia njia potovu kujipatia mamlaka kisiasa.

Kusafirisha wageni kupiga kura ni kuingilia uchaguzi huru, wanasiasa husika wanafaa wakabiliwe vilivyo.

Ni haki ya kila mwananchi kuchagua kiongozi katika mazingira tulivu, salama na kupitia njia ya haki na uwazi.

Pia, anayo haki kulindwa dhidi ya wanasiasa wenye kushiriki siasa chafu za kuponza juhudi za wananchi kuchagua kiongozi wamtakaye bila kuingiliwa.

Kuleta watu wageni kupiga kura ni kutishia haki yao, na wanasiasa husika wanafaa wakabiliwe vilivyo.

  • Tags

You can share this post!

KAMAU: Kiboko kirejee shuleni ili kuboresha nidhamu

AKILIMALI: Ndizi za kienyeji zinazopendwa kwa sukari yake

T L