• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa sharti wachague kwa makini msamiati wanaotumia kutafuta kura

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa sharti wachague kwa makini msamiati wanaotumia kutafuta kura

Na KINYUA BIN KING’ORI

HIKI ndicho kipindi ambacho wanasiasa wanafaa kuwa wajasiri kuhakikisha wanatumia kampeni zao kujenga amani na umoja miongoni mwa Wakenya.

Kampeni za 2022 zimechacha huku visa vya wanasiasa wanaotoa matamshi ya chuki na uchochezi vikizidi kuongezeka.

Wiki jana Seneta wangu wa Meru Mithika Linturi akihutubu katika mkutano wa UDA, Eldoret alitoa matamshi yaliyozua mdahalo nchini kwa kutumia misamiati ‘madoadoa’.

Kwa kuwa matamshi yake yalichukuliwa kuwa yanachochea chuki na uhasama baina ya wafuasi wa Naibu Rais William Ruto na wakosoaji wake Bonde la Ufa, alikamatwa na kushtakiwa.

Wanasiasa hawastahili kutumia kampeni na uchaguzi wa Agosti 9, 2022 kuchochea chuki kisiasa au kikabila.

Aidha, hawapaswi kutumia misamiati inayokumbusha Wakenya masaibu na mateso waliyopitia katika ghasia zilizokumba taifa hili baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Huenda ikawa Seneta Linturi hakumaanisha watu wa makabila mengine wasiomuunga mkono Dkt Ruto kuchukuliwa kama maadui kisiasa eneo hilo, hata hivyo alikosea kutumia neno ‘madoadoa’.

Kuna misamiati ya kisiasa kama vile kuomba wananchi kuchagua viongozi katika mfumo wa ‘suti’ (six piece).

Viongozi wanafaa wajue misamiati bora wanayofaa kutumia katika matamshi yao ili kuzuia taharuki nchini ya kwa kueleweka visivyo.

Matamshi ya Linturi yalikuwa ya kisiasa tu ili kufurahisha wafuasi wa UDA lakini yamekuwa pigo kwa chama hicho Bonde la Ufa na Kenya kwa jumla, maana imeeleweka chama hicho hakivumilii watu wenye maoni tofauti.

Hata UDA ipate nyadhifa zote za kisiasa katika uchaguzi ujao, watajivunia nini ikiwa kuchaguliwa kwao kutachochea chuki kisiasa?.

Je, Dkt Ruto atanufaika kivipi ikiwa atakuwa Rais wa nchi yenye migawanyiko na uhasama wa kisiasa na kikabila?

Je, ataweza vipi kutimiza ajenda yake ya ‘Bottom up’?.

Kenya ni nchi iliyokumbatia mfumo wa vyama vingi, hivyo watu wa Rift Valley ni haki yao kuchagua viongozi watakao bila kuzingatia chama cha UDA.

Hata watu wa Nyanza watachagua viongozi wao kwa sera wala siyo kuegemea Azimio la Umoja lake Raila Odinga.

Huu ndio wakati wa asasi husika Serikalini kutoa ‘makucha’ yao kwa kusuka mbinu bunifu kuwakabili kisheria wanasiasa wanaotoa matamshi kiholela.

Wachochezi wote wakabiliwe bila upendeleo ili kulinda wanasiasa watundu wasitumie siasa kuangamiza taifa hili.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Mashambulio yazimwe kabla kuenea kwingine

Shule za upili kuorodheshwa kwa uwezo wa CBC

T L