• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
KINYUA KING’ORI: Tujadili mbinu za kukabili changamoto zinazotulemea tuache porojo za Agosti 9

KINYUA KING’ORI: Tujadili mbinu za kukabili changamoto zinazotulemea tuache porojo za Agosti 9

NA KINYUA KING’ORI

NASHINDWA kuelewa jinsi “ufichuzi” wa Raila Odinga kushinda kura ya urais katika uchaguzi mkuu uliopita, utakavyotusaidia kukabiliana na ukame unaoshuhudiwa nchini.

Je, manufaa ya ufichuzi huo ni nini iwapo hautasaidia Wakenya kupata maji safi?

Je, madai ya Rais William Ruto kwamba kulikuwa na njama ya kumteka nyara na kumuua aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati, yatamfaa nini raia anayezidiwa na ugumu wa maisha?

Je, madai hayo yatalipia wazazi karo ya watoto wao na kuwanunulia vifaa vya shule?

Je, Rais atatimiza ahadi zake katika muda ufaao ikiwa anatumia muda mwingi kupiga gumzo za uchaguzi mkuu na jinsi mtangulizi wake, Bw Uhuru Kenyatta, alikula njama kuvuruga matokeo ili asitangazwe mshindi?

Rais Ruto atambue gharama ya maisha imekuwa ngumu zaidi na Wakenya watachoka na hizo ahadi zake za kila mara.
Matumaini yao yakififia watampuuza na kukosa imani na serikali yake, jambo ambalo mwishowe litamponza kisiasa.

Viongozi wetu wazingatie uzalendo, wazamie kupata suluhu ya mambo yanayotusonga waache kutuchosha na porojo za siasa.

Sisemi wanaohusishwa na njama za kuvuruga matokeo ya uchaguzi wasiwajibike.

La hasha! Wachunguzwa kwa kina na wakipatikana na hatia wachukuliwe hatua kali ili kuzuia njama zozote chaguzi zijazo.
Ruto ataimarisha asasi zetu akiacha kupiga siasa kuhusu kazi zao.

Vilevile, atekeleze ahadi zake kimyakimya kama mwendazake Mwai Kibaki, aliyekuwa mchache wa gumzo lakini mchapakazi.

Nao upinzani ukiongozwa na Bw Raila Odinga uzingatie kuweka uzito katika mbinu mbadala za kukomboa uchumi wetu, kubomoa mizizi ya ukabila na kuboresha asasi za taifa ili zitimize majukumu yao ipasavyo.

Viongozi wetu wajue siasa za uzushi hazitafaidi taifa bali zitavuruga juhudi za kufufua uchumi na kuimarisha maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

JURGEN NAMBEKA: Kaunti nyingine Pwani ziige ‘Mombasa...

MWALIMU WA WIKI: Martin Gitonga

T L