• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
WASONGA: Likizo si suluhu, ni sawa na kutibu malaria na panadol

WASONGA: Likizo si suluhu, ni sawa na kutibu malaria na panadol

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine, serikali kupitia wizara ya Elimu imeamua kushughulikia kero la utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi kwa njia isiyoridhisha.

Kwa mfano, mnamo Jumanne wizara ya elimu ilichukua hatua ya kushtukiza kwa kuitikia wito wa walimu wakuu wa shule za upili kwamba wanafunzi wapewe likizo fupi.

Kulingana na wasimamizi hao wa shule, hatua hii ndio itazuia visa vya wanafunzi kuzua rabsha na kuteketeza mali ya shule.

Walimu hao wakuu wanadai visa hivyo vinachangiwa na hali kwamba wanafunzi wamechoka baada ya kufupishwa kwa likizo kufidia muda ambao wanafunzi walipoteza mwaka 2020 shule zilipofungwa kufuatia mlipuko wa janga la corona.

Lakini ukweli ni kwamba hatua ya kuwapa wanafunzi likizo ya siku nne pekee (kuanzia Novemba 19 hadi Novemba 23) sio suluhu kamili ya kero hii ya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi.

Hii ni sawa na kumpa mgonjwa wa malaria dawa aina ya panadol (ya kutuliza maumivu).

Kimsingi, kando na walimu wakuu kupendekeza likizo fupi, wangeishinikiza wizara ya elimu iwape fedha za kutekeleza mapendekezo ya jopo kazi lililochunguza kiini cha ghasia hizo za wanafunzi mnamo 2016.

Jopo kazi hilo lililoongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mashariki Bi Claire Omollo, lilibuniwa na aliyekuwa Waziri wa Elimu Fred Matiang’i baada ya shule 107 kote nchini kushuhudia visa vya uteketezaji mabweni.

Kwanza, wizara ya elimu ilitakiwa kubuni idara za kutoa ushauri nasaha haswa katika shule za upili za mabweni.

Hii ni baada ya kubainika kuwa visa hivyo huchangiwa na utovu wa maadili miongoni mwa wanafunzi, matumizi ya pombe na mihadarati, uabudu wa shetani.Lakini kwenye mahojiano katika runinga moja Jumanne usiku Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Shule za Msingi Nchini (Kessha) Kahi Indimuli alikiri kuwa nyingi za shule za upili hazina idara za kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi.

Alieleza kuwa kubuniwa kwa idara kama hiyo kunahitaji ufadhili kutoka kwa serikali, jambo ambalo halijafanyika kufikia sasa.

Lakini akirejelea mapendekezo ya jopokazi hilo la Bi Omollo, Bw Indimuli alilaumu wazazi kwa kutelekeza wajibu wao kama walezi wa watoto na kuachia walimu wajibu huo.

Japo kauli hiyo ina mashiko, utepetevu miongoni mwa walimu wakuu pia ulitajwa kuwa chanzo cha kutokea kwa fujo shuleni.

Jopokazi hilo lilibaini kuwa baadhi ya walimu wakuu huwa hawashughulikii malalamishi ya wanafunzi haraka, hali inayochangia wao kuzua ghasia ili shida zao zishughulikiwe.

Hii ndio maana ilipendekezwa kwamba walimu wakuu wa shule za upili za mabweni waishi ndani ya shule au maeneo ya karibu ili waweze kufuatilia mienendo ya wanafunzi haraka.

Bila shaka kupitia viranja wa wanafunzi walimu wakuu wanaweza kupata taarifa kuhusu manung’uniko yao na kuyashughulikia kwa haraka badala ya kusubiri uharibifu wa mali kutokea.

Kwa hivyo, japo likizo fupi ni njia mojawapo ya kukabili tatizo hili, hatua hii haitoi suluhu la kudumu.

Mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya jopokazi la Bi Omollo yatekelezwe.

  • Tags

You can share this post!

AKILIMALI: Alikuwa jamaa la kubeba mizigo; sasa ana...

DOMO KAYA: Ukimya ni dhahabu…!

T L