• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
WANDERI KAMAU: Mataifa yaungane kukabili Omicron, sio kulaumiana

WANDERI KAMAU: Mataifa yaungane kukabili Omicron, sio kulaumiana

Na WANDERI KAMAU

TANGU janga la virusi vya corona kugunduliwa na kuvuruga mfumo wa kimaisha katika karibu nchi zote duniani, kumekuwa na hali ya kutoaminiana baina ya nchi kuhusu jinsi mikakati ya kulikabili inavyoendeshwa.

Malalamishi hayo yalianza kujitokeza mwanzoni mwa mwaka huu 2021, baada ya nchi kama Amerika na Uingereza kufaulu kupata chanjo za mwanzo dhidi ya virusi hivyo.

Baada ya kufaulu kupata chanjo hizo, mataifa hayo mawili na mengine yenye utajiri mkubwa yalisema yatawapa kipaumbele raia wao kwenye juhudi za kuzisambaza.

Hata hivyo, ni hatua iliyozua ghadhabu kubwa miongoni mwa nchi maskini na zile zenye ukuaji wa kadri— ambapo zilidai kubaguliwa kwenye usambazaji wake.

Baadhi ya nchi hata zimekuwa zikilaumiwa kwa kuficha chanjo na kuziuza kwa bei ghali kwa mataifa ambayo bado hayana uwezo mkubwa wa kifedha kuzinunua.

Mataifa ambayo yamekuwa yakilalamika sana ni yale yaliyo barani Afrika, barani Asia na eneo la Carribean.

Ingawa ni jambo ambalo lilionekana kuepukwa na mataifa yaliyoelekezewa lawama, cha kushagaza ni kuwa limejirudia tena baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza kugunduliwa kwa aina mpya ya corona inayoitwa ‘Omicron.’

Virusi hivyo viligunduliwa nchini Afrika Kusini majuma mawili yaliyopita, hali ambayo imezua hofu kote duniani.

Kulingana na WHO, virusi hivyo ni hatari ambapo kinyume na aina za hapo awali, vinasambaa kwa kasi sana.

Bila shaka, ugunduzi huo umezua mdahalo mkubwa, baada ya Afrika Kusini kujitokeza wazi kulalamika kuwa “inaonewa” na baadhi ya mataifa ya Ulaya.

Kauli ya taifa hilo inatokana na hatua ya nchi hizo kusimamisha ghafla safari za ndege kuelekea ama kutoka Afrika Kusini, bila hata kutoa nafasi kwa watu kujitayarisha kukabiliana na athari za tangazo hilo.

Bila shaka, ni jukumu la msingi kwa taifa lolote lile kuwalinda raia wake dhidi ya janga lolote.

Hata hivyo, ‘ulinzi’ huo haupaswi kuendeshwa kwa utaratibu unaoonekana kukuza ubaguzi ama kuamsha uhasama wa kisiasa wa jadi baina ya nchi mbalimbali.

Ni wazi kuwa hata baada ya nchi nyingi za Afrika kujinyakulia uhuru kutoka kwa Wazungu, bado kuna hali ya mivutano na kulaumiana baina ya pande hizo mbili.

Kwa mfano, nchini Afrika Kusini, inadaiwa kuwa hali ya umoja na ushirikiano bado haijawahi kurejea kati ya Waafrika na Wazungu kutokana na dhuluma ambazo Waafrika wengi walipitia enzi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Wasomi wanadai huenda ni hatua hiyo inayoyasukuma baadhi ya mataifa ya Ulaya kutoa marufuku za usafiri dhidi ya Afrika Kusini kama njia ya ‘kulipiza kisasi.’

Katika nyakati hizi ngumu, ni makosa makubwa kwa nchi yoyote ile kufufua uhasama wa jadi kwa kisingizio cha “kulipiza kisasi” dhuluma za jadi.

Mivutano kama hiyo haitamfaidi yeyote, bali itahatarisha afya za raia wa nchi hizo na kujenga uhasama usiofaa.

Ukoloni-mamboleo ni mbinu iliyopitwa na wakati.

Wito wetu ni kwa nchi zote kusahau uhasama wa jadi na kuungana pamoja kulikabili janga hilo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mlofa mwizi ajuta baada ya simu kuita jina la mwenyewe

Real Madrid yakung’uta Bilbao na kufungua mwanya wa...

T L