• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
STEVE ITELA: Ni jukumu letu sote kuwalinda wanyamapori tunapotumia barabara zetu

STEVE ITELA: Ni jukumu letu sote kuwalinda wanyamapori tunapotumia barabara zetu

Na STEVE ITELA

MIUNDO msingi ya Uchukuzi kama vile reli, barabara na nguzo za kupitisha stima huchangia ustawi wa kiuchumi wa taifa na eneo zima kwa jumla, utamaduni na kijamii pamoja na utangamano.

Katika miaka ya hivi majuzi, Kenya imeshuhudia ukuaji na upanuzi wa kiwango ambacho hakikutarajiwa katika miundo msingi ya uchukuzi. Ustawi huu wa haraka unatokana na sera kama vile Ruwaza ya Mwaka 2030 na Ajenda Kuu Nne.

Kwa mfano, sasa hivi kuna kilomita 117,800 za barabara ya lami kote nchini. Ukuaji huu umeshuhudia ongezeko kubwa la magari barabarani. Athari kwa mazingira kutokana na upanuzi huu wa barabara ni nyingi, vikiwemo vifo vya wanyamapori kwa kugongwa na magari.

Visa kadhaa vya wanyamapori kuuawa barabarani vimerekodiwa na wasafiri, madereva, wakazi na watalii wanaotumia barabara zetu. Mauaji haya ya wanyamapori wakati mwingine huibua hisia za umma na shinikizo lakini hiyo haitoshi.

Watumiao barabara na wenye magari wanahatarisha idadi na aina za wanyamapori na wanafaa kuwa waangalifu zaidi.?Isitoshe, kuuawa kwa wanyamapori barabarani pia kunaweza kuathiri maisha ya wanadamu ukiwemo usalama na afya zao.

Ipo haja ya kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa deta na takwimu kuhusu wanyamapori tulio nao na jinsi ya kuwalinda dhidi ya madereva wasio waangalifu. Limekuwa jambo la kawaida siku hizi hapa Kenya kusoma, kusikia au kuona habari kuhusu vifo vya wanyamapori kwenye barabara zetu.

Hili ni jambo linalotia wasiwasi. Mamlaka ya Barabara Kuu Nchini (KENHA) yapaswa kuweka alama barabarani katika maeneo kama hayo. Sote tuchukue jukumu hili la kuwalinda wanyamapori. Ni urathi wetu wa kitaifa.

Bw Itela ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Conservation Alliance of Kenya.

You can share this post!

Ujanja mpya wa kampeni za Raila, Ruto

Sharti uchaguzi uwe wa amani -Matiang’i

T L