• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Ujanja mpya wa kampeni za Raila, Ruto

Ujanja mpya wa kampeni za Raila, Ruto

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaonekana kuendeleza mbinu za kampeni za kulambana visigino wakisaka uungwaji mkono maeneo mbalilmbali nchini.

Kila mmoja amekuwa akifuata mwenzake katika ziara zao maeneo mbalimbali nchini katika kile kinachoonekana kama kupimana nguvu kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.Kwa mfano, mwishoni mwa wiki jana, Dkt Ruto alifanya ziara ya siku tatu katika kaunti ya Nyeri siku chache baada ya Bw Odinga kutembelea eneo hilo akiandamana na ujumbe wa wazee wa jamii ya Waluo.

Hii ilionekana kama mbinu ya kukabili mpenyo wa Bw Odinga katika kaunti hiyo na eneo zima la Mlima Kenya; ambalo, kwa muda mrefu, Dkt Ruto ameonekana kulidhibiti.Kiongozi huyo wa ODM amekuwa akichangamkiwa pakubwa katika eneo hilo tofauti na hali ilivyokuwa katika chaguzi za hapo awali, hali ambayo imeiwatia hofu washirika wa Dkt Ruto katika eneo hilo.

Hii ni kwa sababu katika ziara zake katika eneo hilo, anazotaja kama jaribio lake la kuukwea Mlima Kenya, Bw Odinga huandamana na magavana kadha, wakiongozwa na mwenyekiti wa muungano wa magavana eneo hilo, Francis Kimemia.Pia, amekuwa akiandamana na baadhi ya mawaziri wa serikali kuu na mabwanyenye kutoka eneo hilo wakiongozwa na mmiliki wa shirika la utangazaji la Royal Media Services SK Macharia.

Baada ya ziara ya kiongozi huyo wa ODM Nyeri, baadhi ya wabunge wandani wa Dkt Ruto walidai idadi kubwa ya watu waliohudhuria mikutano yake walisafirishwa kutoka Nyanza.Hata hivyo, gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alipuuzulia mbali madai hayo, akishikilia kuwa watu wote waliojitokeza kumlaki Bw Odinga katika maeneo bunge mbalimbali alikozuru “ni wakazi asilia wa kaunti ya Nyeri.

”?Mnamo Novemba 21, Bw Odinga naye alifululiza hadi pwani kwa ziara ya siku tatu wiki mbili baada ya Dkt Ruto kutifua kivumbi katika eneo hilo kuuza sera zake za kuwainua walalahoi kuichumi.Kiongozi huyo wa ODM alizuru kaunti za Lamu, Kilifi na Kwale ambako Naibu Rais pia alitembelea kujipigia debe.

Kambi ya Bw Odinga ilionekana kuingiwa na kiwewe kutokana na ziara ya kila mara ya Dkt Ruto katika eneo hilo linaloaminika kuwa ngome ya chama cha ODM.Wawili hao walionekana kufuatana katika kampeni, kila mmoja akipania kunyakua jumla ya kura 1.7 milioni za eneo hilo.

Katika ziara yake kaunti ya Lamu, Bw Odinga alionekana kumuiga Dkt Ruto alipopanda punda, mnyama anayetumika katika shughuli za uchukuzi eneo hilo.Kaunti hiyo yenye idadi ya wapiga kura 69,774 ni muhimu kwa Bw Odinga kwa sababu ina idadi kubwa ya wapiga kura kutoka jamii ya Wakikuyu katika eneo la Mpeketoni.

You can share this post!

Ujenzi wa Uhuru Park wasimamishwa

STEVE ITELA: Ni jukumu letu sote kuwalinda wanyamapori...

T L