• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
CECIL ODONGO: ODM isipotoshwe mkono wa Rais ushafikisha Raila ikulu

CECIL ODONGO: ODM isipotoshwe mkono wa Rais ushafikisha Raila ikulu

Na CECIL ODONGO

IMANI inayoendelea kujengeka miongoni mwa wafuasi wa ODM kuwa Kinara wao Raila Odinga tayari ameshinda kiti cha urais kutokana na uungwaji mkono wa Rais Kenyatta ni hatari.

Ingawa hajatangaza hadharani kuwa anamuunga mkono Bw Odinga, matukio mbalimbali yamekuwa yakionyesha kuwa huenda kiongozi wa nchi yupo nyuma ya waziri huyo mkuu wa zamani.

Wikendi, Rais Kenyatta aliivunja itifaki na kumruhusu Bw Odinga akahutubu baada yake siku ya Jamuhuri katika uga wa Uhuru Gardens, tukio ambalo si kawaida tangu nchi ijinyakulie uhuru.

Mara tu baada ya kisa hicho, wafuasi wa ODM walijibwaga mtandaoni wakifasiri hatua hiyo kuwa Rais Kenyatta anaendelea kumpiga kumbo naibu wake Dkt William Ruto na Bw Odinga sasa yupo guu moja tu kuingia ikulu.

Baadhi hata waliandika kuwa sasa kilichosalia ni kusaka uwanja ambao utatosha halaiki ya watu ambao watajitokeza kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Bw Odinga, wakidai hakuna uwanja ambao unatosha nchini na hata ikiwezekana utafutwe ng’ambo, wakisisitiza wana uwezo wa kusafiri huko kushuhudia ‘tukio’ hilo la kihistoria.

Mbali na hayo, mawaziri kadhaa pamoja na maafisa wengine wa utumishi wa umma, walihudhuria hafla ya Azimio la Umoja katika uga wa Kasarani, Ijumaa iliyopita, ambako Bw Odinga alitangaza kuwa atawania kiti cha Urais kwa mara ya tano.

Ishara nyingine inayosababisha watu wa ODM waamini kuwa Bw Odinga ashaingia ikulu ni jinsi ambavyo amekuwa akiandamana na Rais Kenyatta kwenye hafla ya kuzindua miradi mbalimbali nchini.

Vilevile mapokezi ya kishujaa ambayo kigogo huyo wa siasa za upinzani amekuwa akipata katika eneo la Mlima Kenya ambako hangeweza kutia guu lake 2007,2013 na 2017 kuuza ajenda zake za kisiasa, imesawiriwa na wafuasi wa ODM kuwa nafasi ya Bw Odinga ya kuingia ikulu sasa imetimia.

Hata hivyo, wafuasi wa ODM wanafaa waje polepole kwa sababu mwanzo hakuna anayefahamu kuwa aidha Bw Odinga au Ruto watafikia 2022 kwa sababu mwenyezi mungu ndio ana ufunguo wa maisha.

Pili, jinsi wanavyojitanua na kujigamba mitandaoni huenda ikahofisha baadhi ya jamii kumpigia kura Bw Odinga 2022. Badala yake wanafaa wanyenyekee na kumsaidia Bw Odinga kuwashawishi watu hasa wa Mlima Kenya wamuunge mkono.

Tatu, imani kuwa kuna ushawishi na kuwa Bw Odinga ashapita kura huenda ikasababisha baadhi wasijitokeze siku ya kupiga kura.

Kwa mujibu wa wana ODM, Bw Odinga amekuwa akishinda uchaguzi, 2007, 2013 na 2017 ila kutokana na kupingwa na baadhi ya watu serikalini, amekuwa akipokonywa ushindi huo.

Kwa hivyo kutokana na ushirikiano kati ya Rais na nyapara wao, wanaamini kigogo huyo asihinde au asishinde bado atatangazwa mshindi 2022.

Hata hivyo imani hii inaipaka tope IEBC kama tume ambayo haina uhuru kiutendakazi.

Pia inaisawiri kama inayopendelea utawala uliopo na huenda kura ya 2022 haitashirikisha uamuzi wa Wakenya wengi.

Takwimu za IEBC kuhusu usajili wa wapigakura inaonyesha kuwa ngome za Dkt Ruto na Bw Odinga walijisajili kwa kiwango cha wastani.

Kwa hivyo, ni mbinu za kampeni za kila moja wao, ndizo zitahakikisha mmoja wao anachaguliwa 2022 bali si mmoja kuungwa mkono na serikali au la.

  • Tags

You can share this post!

Mrithi wa Uhuru kubeba zigo zito

Wito watu wapime kansa ili kupunguza ada za kutibu

T L