• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
CHARLES WASONGA: Serikali ifadhili mpango wa kushauri polisi wanaotaabika

CHARLES WASONGA: Serikali ifadhili mpango wa kushauri polisi wanaotaabika

CHARLES WASONGA

IPO haja kwa serikali kuu kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia visa vya maafisa wa polisi kujiua au kuua watu wengine, wakiwemo jamaa zao.

Hii ni kwa sababu tayari visa hivi vimesababisha hofu miongoni mwa maafisa hao wenyewe, wakubwa wao, familia zao na Wakenya kwa ujumla.

Kimsingi, polisi wanapaswa kutumia bunduki zao kwanza kulinda maisha yao, dhidi ya wahalifu, wakiwa kazini pamoja na pili kulinda mali na maisha ya Wakenya ambao wameajiriwa kuwahudumia.

Lakini inatamausha, na kuvunja moyo, kwamba nyakati hizi kuna ongezeko la visa vya maafisa wa polisi kujitoa uhai au kuwaua watu wa familia zao kwa njia za kutatanisha.

Kisa cha hivi punde kilitokea wiki jana ambapo afisa wa polisi aliyetambuliwa kwa jina, Benson Imbatu aliwaua watu sita katika eneo la Kabete kabla ya kutumia bunduki hiyo kujiua.

Afisa huyo alipiga risasi mkewe, watoto wake na wahudumu watatu wa bodaboda waliofika katika makazi kushuhudia kilichokuwa kikitendeka.

Akigusia kisa hicho, Rais Uhuru Kenyatta aliwashauri maafisa wa polisi wanaozongwa na hali ngumu, kuwapasha habari wakubwa wao au watu wa familia zao badala ya kuua na kujiua.

Akihutubu alipoongoza hafla ya kufuzu kwa maafisa wa kikosi cha polisi wa kupambana na fujo (GSU) katika chuo cha mafunzo yao eneo la Embakasi, Nairobi, Rais Kenyatta aliungama kuwa kuna baadhi ya maafisa wa polisi wanaozongwa na matatizo ya kiakili.

Lakini kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini, nahisi kwamba Rais Kenyatta alipaswa kutangaza bayana jinsi serikali yake inashughulikia tatizo hilo.

Haitoshi kwa kiongozi wa taifa kuwashauri maafisa waathirika, na tena hadharani, kuwasilisha matatizo yao kwa wakubwa wao na familia zao.

Hii ni kwa sababu siri iliyo wazi ni baadhi ya maafisa wa polisi huamua kuchukua sheria mikononi mwao kwa sababu ya kudhulumiwa na wakubwa wao.

Kwa mfano, baadhi ya maafisa hudai kuhamishiwa maeneo yenye mazingira magumu ya kufanyia kazi au kutopandishwa vyeo baada ya kuhudumu kwa miaka mingi.

Vile vile, kumekuwa na malalamishi mengi, haswa kutoka kwa maafisa wa vyeo vya chini, ambao hudai wakubwa wao huwanyima ruhusa ya kwenda nyumbani kushughulikia matatizo yao ya kifamilia, kunyimwa nafasi ya likizo ya masomo.

Masuala hayo, na mengine mengi, yamejitokeza katika chunguzi kadha zilizofanywa na Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC) katika miaka ya nyuma katika juhudi za kutaka kubaini kiini cha visa vya maafisa wa polisi kujiua.

Kwa hivyo, Afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na tume ya NPSC, zishirikiane kuomba ufadhili wa kutosha kutoka bungeni na Hazina ya Kitaifa kwa ajili ya kuanzisha vitengo vya ushauri nasaha katika vituo vyote vya polisi nchini.

  • Tags

You can share this post!

Dada wawili kushtakiwa kushambulia pacha

Nasa ulikuwa muungano wa kusaka uongozi 2017, asema Junet

T L