• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
TAHARIRI: Aina mpya ya Covid ikabiliwe isilete lockdown

TAHARIRI: Aina mpya ya Covid ikabiliwe isilete lockdown

KITENGO cha UHARIRI

Wizara ya Afya imetangaza hatari ya aina mpya ya virusi vya corona ambayo imeanza kushambulia mataifa mbali mbali haswa kusini mwa Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa huduma za Afya Dkt Patrick Amoth ametangaza kuwa wasafiri wanaowasili kutoka Botswana na Hong Kong watahitajika kupimwa kuthibitisha kwamba hawana virusi hivyo huku akisema aina hiyo mpya inasambaa kwa haraka zaidi hata kuliko ile aina ya Delta ambayo ilitikisa mataifa mengi ikiwemo Amerika.

Aidha, aina hiyo mpya inasemekana kuwa isiyosikia nyingi ya chanjo ambazo zimekuwa zikitolewa kwa umma, jambo linaloibua wasiwasi kwamba huenda zile ziku ngumu za kuwekewa vikwazo au ‘lockdown’ zikarudi tena wakati ambapo wengi wameshachukulia kuwa janga hilo limekwisha.

Lakini kama tulivyojifunza katika karibu miaka miwili ya janga hili kufikia sasa, mbinu za kupambana zingali zile zile rahisi ambazo zinahusu kila mmoja wetu kufanya jukumu lake. Serikali na asasi zake zikaze kamba katika upekuaji na upimaji katika vituo vyote vya mpakani na kufuatilia visa vyote vinavyoshukiwa pamoja na kutoa huduma bora hospitalini, huku wananchi nao wakiendelea kuvalia barakoa, kunawa mikono na maji safi ya kutiririka kila mara na kudumisha umbali na haswa kuepuka mikutano mikubwa ya watu.

Inatia moyo kwamba makahama imekubaliana na serikali kuhusu shinikizo la kuhakikisha watu wengi wanapokea chanjo iwezekanavyo. Kama wanavyosema wanasayansi, chanjo ndiyo silaha kamili ya janga hili haswa kama idadi kubwa ya watu; hadi kufikia asilimia 90 watapata chanjo.

Mnamo Novemba 21 2021, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitoa ilani kwamba yeyote ambaye hajachanjwa atanyimwa huduma katika afisi za serikali, jambo lililozua malalamishi yaliyoishia mahakamani. Lakini Jaji Anthony Mrima jana alikataa kuondoa ilani hiyo akisema anataka kusikia mawasilisho kutoka pande zote kwanza.

Sote tulishuhudia jinsi vikwazo na lockdown zilivyosambaratisha sehemu kubwa ya maisha ya kawaida humu nchini. Wengi walipoteza ajira, wengi wakaathirika kifedha, kisaikolojia na kijamii. Na sasa tunakodolea macho hatari ya kurudishwa katika enzi za kafyu endapo hatutajishughulisha ipasavyo kupiga breki aina hiyo mpya kabla imee mizizi humu nchini.

Kwa hivyo, ni jukumu letu kuepuka mikutano ya hadhara haswa hii ya kisiasa. Kwa kweli, hakuna chochote cha maana mwanasiasa atakuambia kwenye mikutano hiyo ambacho hutakipata kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii kwa hivyo hamna haja kuhatarisha kupatwa na corona mpya sababu ya siasa.

You can share this post!

Mzee Oroni bado anatimua mbio hafikirii kustaafu licha ya...

Ruto asusia Kongamano la Ugatuzi

T L