• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
TAHARIRI: Dereva, abiria washirikiane kuzuia ajali msimu huu

TAHARIRI: Dereva, abiria washirikiane kuzuia ajali msimu huu

KITENGO cha UHARIRI

MKASA wa basi kuzama na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 23 katika mto Enziu ni funzo kwa Wakenya msimu huu wa sherehe ambapo wengi watakuwa wakisafiri kutoka mijini kuelekea mashambani kujumuika na jamaa zao.

Wengine watakuwa wakisafiri kuelekea pwani ya Kenya na maeneo mengine ya starehe kusherehekea Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya. Hivyo basi, ipo haja kwa wananchi kuwa makini zaidi na wakome kuabiri mabasi na matatu ambayo hayajazoea kutumia barabara fulani ili kuzuia mkasa sawa na ule ambao ulitokea Mwingi juzi kwa sababu ilidhihirika wazi kuwa dereva hakuwa na ufahamu mzuri wa barabara hiyo.

Isitoshe, abiria wa basi walidaiwa kumshinikiza dereva wao kuwavusha baada ya kuona magari mengine mawili yakivuka kwa ufanisi mkubwa.Wakati kama huu baadhi ya matatu zinazohudumu katika barabara za Nairobi na maeneo ya karibu huamua kubeba abiria wa kuelekea magharibi mwa Kenya au maeneo ya Mlima Kenya kutokana na ongezeko la abiria wanaosafiri mashambani.

Japo hii ni kinyume cha sheria za Bodi ya Kutoa Leseni kwa Magari ya Uchukuzi (TLB) wahudumu wa magari hayo hutoa hongo kwa maafisa wa trafiki na hivyo kukwepa adhabu.Ni rahisi kwa madereva kama hawa kusababisha ajali kwa kukosa ufahamu wa hali ya barabara za maeneo ya mashambani haswa katika msimu huo wa mvua nyingi.

Pili, ni wakati kama huu ambapo magari mengi huamua kubeba abiria wengi kupita kiasi na madereva kuendesha kwa kasi ya juu ili kuvuna faida kubwa.Wananchi ambao watakuwa wakisafiri kutoka mijini kuelekea maeneo ya mashambani kujumuika na wapendwa wao kwa sherehe mbalimbali waepuke magari kama haya.

Isitoshe, raia wakome kutumia magari ya kibinafsi ambayo hayana leseni ya kuyaruhusu kubeba abiria. Magari kama hayo ni hatari kwa usalama na maisha yao.Kulingana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) Septemba 21 mwaka huu, idadi ya watu waliofariki katika ajali za barabarani iliongezeka hadi 3,975 mwaka jana kutoka 3,586 mnamo 2019.

Hii ni licha ya kwamba serikali ilikuwa ikitekeleza masharti makali ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa hatari kama vile kafyu na marufuku ya kusafiri.Sote tunapaswa kusaidiana kuzuia ajali barabarani katika msimu wa sikukuu

You can share this post!

Sababu za Rais ‘kuhepa’ mkutano wa Raila- Wadadisi

PAA kuhudhuria mkutano wa Raila Kasarani

T L