• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
TAHARIRI: Gavana Mwangaza asafiane nia na madiwani wake

TAHARIRI: Gavana Mwangaza asafiane nia na madiwani wake

NA MHARIRI

BUNGE la Kaunti ya Meru limemulikwa hivi majuzi wakati madiwani wote waliondoka bungeni punde tu Gavana Kawira Mwangaza aliposimama kuwahutubia, ni dalili za mapema za uhasama baina ya pande zote mbili za uongozi wa kaunti.

Wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika bunge hilo ,Bw Evans Mawira, walimsuta Gavana kwa kuwadharau, kuwatenga na kujaa kiburi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Cha kusikitisha ni kwamba Gavana Mwangaza anasingizia madiwani kuingiza siasa katika sula nzima, ili aepuke madai ya kuajiri familia yake katika nyadhifa za kaunti.

Jamaa zake hao ni mumewe Murea Baichu na dada zake wawili, madai ambayo hata Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inachunguza. Magavana wajue wao si wafalme kutaka kuendesha kaunti kama himaya zao za utawala pasipo kushirikisha viongozi wengine.

Tangu serikali za kaunti kuanzishwa 2013 tumeona baadhi ya magavana na madiwani wao wakilumbana muhula mzima bila sababu maalum ila kiburi na ujeuri wa mamlaka.

Wananchi wa Meru walimchagua Gavana Mwangaza na madiwani wao kwa misingi kwamba viongozi hao watashirikiana kuwainua kiuchumi na kuleta maendeleo. Malumbano kama haya yalisambaratisha serikali za magavana wengi nchini huku madiwani wakilalamikia kutohusishwa katika uteuzi wa miradi ya kutekelezwa katika wadi.

Namsihi Gavana Mwangaza aache kujipiga kifua eti anaonyesha madiwani nani mwenye kusema katika kaunti. Ndiye Gavana wala hakuna atakayempokonya hilo kwa sasa.

Hata hivyo, kiburi kitamponza na ataishia kuwa Gavana bwege au hata kuondolewa mamlakani akipatikana na hatia ya kuvunja sheria ya uteuzi.

Madiwani wa Meru wanayo haki ya kukosoa utawala wa kaunti, na Gavana hana budi kukubali hilo. Azingatie kutimiza ahadi zake kwa raia na hilo litafanyika tu iwapo atakuza ushirikiano na unyenyekevu katika uongozi wake.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Hofu ya Ruto ‘kutekwa’ na mawaziri...

MIKIMBIO YA SIASA: Kwa mkakati huu, Sakaja yuko vizuri!

T L