• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
JUNGU KUU: Hofu ya Ruto ‘kutekwa’ na mawaziri rafiki zake

JUNGU KUU: Hofu ya Ruto ‘kutekwa’ na mawaziri rafiki zake

NA WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto anakabiliwa na kibarua kigumu kutimiza ahadi alizotoa kwa Wakenya, baada ya baraza lake la mawaziri kuapishwa rasmi hapo Alhamisi.

Licha ya matumaini mengi yaliyopo, wadadisi wa siasa wanasema mtihani mkuu unaomkabili Dkt Ruto ni kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni, ikizingatiwa mawaziri wengi aliowateua ni wanasiasa na marafiki wake wa karibu.

Kulingana nao, kibarua kinachomkabili Dkt Ruto ni kuhakikisha mawaziri hao hawatumii nyadhifa hizo kujijenga kisiasa, kwani huenda baadhi yao wakarejea siasani kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Baadhi ya mawaziri wanasiasa walioapishwa ni aliyekuwa Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen, wabunge Aden Duale (Garissa Mjini) na Alice Wahome (Kandara).

Bw Murkomen aliteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi na Barabara, Bw Duale kama Waziri wa Ulinzi huku Bi Wahome akiteuliwa kama Waziri wa Maji. Wadadisi wanaeleza hofu aliyo nayo Dkt Ruto ilidhihirishwa na kauli kali alizotoa wakati wa kuapishwa kwao.

“Ijapokuwa kauli ya Dkt Ruto kwa mawaziri hao ilionekana kama njia ya kuwaambia kujitolea kufanya kazi, kwa upande mwingine iliashiria hofu aliyo nayo kuhusu ikiwa watatimiza malengo aliyo nayo kwao au la,” asema Bw Oscar Plato, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wanasiasa wengine walio katika baraza hilo ni aliyekuwa gavana wa Machakos Alfred Mutua (Mashauri ya Kigeni), mbunge wa zamani wa Malindi, Aisha Jumwa (Utumishi wa Umma), aliyekuwa Mwakilishi wa Kike Kajiado, Soipan Tuya (Mazingira), aliyekuwa Seneta wa Meru Mithika Linturi (Kilimo) miongoni mwa wengine.

Wadadisi wanaeleza kuwa kwa kuwateua washirika wake, Dkt Ruto yuko katika njiapanda, kwani itamlazimu kudumisha urafiki na ushirika wa kisiasa kwa wakati mmoja.

“Wanasiasa wengi walioteuliwa katika baraza hilo ni marafiki wa karibu wa Dkt Ruto. Uteuzi wa baadhi yao ulikuwa kama shukrani kwa usaidizi waliompa wakati wa kampeni zake za kuwania urais. Katika hali hiyo, itakuwa vigumu kuwakosoa, ikiwa watakosa kuwajibika au kupatikana kwenye makosa,” akasema Bw Plato.

Kibarua kinachomkabili Dkt Ruto kinafananishwa na hali aliyojipata Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki katika muhula wa kwanza wa serikali ya NARC, baada ya washirika wake wa karibu kisiasa kuhusishwa na sakata za ufisadi.

Baadhi ya washirika hao ni aliyekuwa Waziri wa Fedha, David Mwiraria, Bw Kiraitu Murungi (Haki na Masuala ya Katiba), Dkt Chris Murungaru (Usalama wa Ndani) na Amos Kimunya (Ardhi).

Mawaziri Mwiraria, Kiraitu na Murungaru walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao, baada ya kuhusishwa na sakata ya Anglo-Leasing.

Bw Kimunya alitajwa kujifaidi kutokana na uuzaji tata wa mkahawa wa Grand Legency kwa serikali ya Libya, wakati huu ikijulikana kama Laico Regency.

“Ijapokuwa Rais Kibaki aliwarejesha kazi baadhi yao baada ya kuondolewa makosa na jopo kadhaa zilizobuniwa kuwachunguza, alifanya hivyo shingo upande, kwani walikuwa washirika na marafiki wake wa karibu kwa miaka mingi katika ulingo wa siasa,” asema mdadisi wa siasa Prof Macharia Munene.

  • Tags

You can share this post!

JAMVI LA SIASA: Ruto angemtumia Kalonzo kuatika mbegu ya...

TAHARIRI: Gavana Mwangaza asafiane nia na madiwani wake

T L