• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
TAHARIRI: Hatua iliyopigwa na Waziri kuhusu kandanda inatia moyo ila kazi bado

TAHARIRI: Hatua iliyopigwa na Waziri kuhusu kandanda inatia moyo ila kazi bado

NA MHARIRI

WAZIRI wa Michezo Ababu Namwamba amekuwa na wiki nzima ya kwanza afisini tangu alipoapishwa kwa wadhifa huo, na kulingana na habari zinazochipuka kutoka ofisi yake, ni wazi kwamba hajakuwa akilaza damu.

Habari za hivi punde ni kwamba serikali imerejesha afisini sekretariati ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF), ambayo ndiyo inatambuliwa katika usimamizi wa soka kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA).

Hatua hiyo inachukuliwa na wadau kuwa mojawapo ya mikakati inayonuiwa kuridhisha shirikisho hilo la dunia, kwamba Kenya inafuata vigezo ilivyowekewa ili kuondolewa marufuku ya kushiriki soka ya kimataifa.

Kufuatia hatua hiyo, Katibu wa FKF Barry Otieno na Makamu wa Rais wa FKF Doris Petra, ambao walikuwa kati ya waliofurushwa na aliyekuwa Waziri Amina Mohamed, wameruhusiwa kurejea afisini.

Hata hivyo, Rais wa FKF Nick Mwendwa amebakia nje hadi mwelekeo utolewe kuhusu kesi inayomuandama mahakamani, inayohusiana na ubadhirifu wa fedha katika shirikisho hilo.

Itakumbukwa kuwa mojawapo ya vigezo vya Fifa ni kwamba lazima uongozi wa FKF – shirikisho ambalo pekee wanalitambua katika usimamizi wa soka – urejeshwe na shughuli za kawaida kuendelea.

Itasubiriwa kuona iwapo hatua ya Waziri Namwamba itatosha kuyeyusha nyoyo za Fifa kuondoa marufuku hayo, ambayo yamevuruga kabisa usakataji wa kandanda nchini.

Tayari klabu za Ligi Kuu (KPL) zimekataa kurejelea msimu mpya wa 2022/2023 iwapo mtafaruku huu hautatatuliwa, kwa sababu wanahisi kwamba haina maana wao kupigania taji ilhali hawatakubaliwa kushiriki mashindano ya haiba kubwa kama CAF ilivyo mojawapo ya motisha kubwa ya kupigania kushinda taji la KPL.

Kinachofuatia ni kwamba wanasoka na wanaotegemea taaluma ya soka wamebakia wakihangaika kutokana na kuchelewa kuanza kwa msimu mpya. Wengi wanakosa marupurupu kwa sababu baadhi ya kandarasi zao zinategemea na mechi walizohusika.

Kwa hivyo, itamjuzu Waziri kuendelea kukaza kamba kwa ushirikiano ambao ameonyesha kufikia sasa ambapo hata pia aliita wakuu wa vilabu ili kujadiliana kuhusu mwelekeo.

Aidha, Kenya haina muda mwingi katika juhudi hizi kwa sababu kufikia Novemba 8, Fifa itahamia Qatar kuzamia maandalizi ya Kombe la Dunia; ikimaanisha kwamba hawatashughulika na jambo lingine lolote hadi dimba hilo litamatike mwezi mmoja baadaye.

You can share this post!

Kichaa cha mbwa chavamia kaunti 8 nchini

DOUGLAS MUTUA: Serikali iipe umuhimu afya ya akili ya...

T L