• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Kichaa cha mbwa chavamia kaunti 8 nchini

Kichaa cha mbwa chavamia kaunti 8 nchini

NA ANGELA OKETCH

KAUNTI nane zimeripoti visa vya kichaa cha mbwa, kulingana na Chama cha Kutetea Afya ya Wanyama (KSCAVA).

Nairobi inaongozwa kwa visa hivyo ikifuatiwa na Nakuru, Kwale, Kilifi, Wajir, Narok na Isiolo.

Juzi, mtoto mmoja aliaga dunia kutokana na matatizo yaliyosababishwa na kichaa cha mbwa katika Kaunti ya Siaya baada ya kuumwa na mbwa.

Katika Kaunti ya Nairobi, visa hivyo viliripotiwa katika eneo la Oloolua, Karen, Runda na Dagoretti.

Katika Kaunti ya Nakuru, maeneo ambayo yameathirika yanajumuisha Naivasha, Keragita na Kambi ya Moto.

Baadhi ya visa pia vimeripotiwa kutokea kwenye Hifadhi ya Maara Kaskazini katika Kaunti ya Narok.

Kichaa cha mbwa husababishwa na virusi ambavyo vinaingia ndani ya mwili wa binadamu anapoumwa na mbwa mwenye maradhi ama kugusa vidonda vya wanyama ambao wameathiriwa.

Bila kupata matibabu ya haraka, maradhi ya kichaa cha mbwa yanaweza kusababisha kifo mara moja baada ya kuambukizwa.

Takwimu zinaonyesha kuwa ugonjwa huu husababisha jumla ya vifo 60,000 kila mwaka hasa katika mataifa yanayoendelea.

Asilimia 36 ya watu hao wanatoka katika bara la Afrika.

Nchini Kenya, takriban watu 2,000 kwa wastani huaga dunia kila mwaka kwa sababu ya kichaa cha mbwa.

Hapo jana Ijumaa, Wizara ya Afya haikuwa imetoa taarifa yoyote kuhusu mkurupuko wa maradhi hayo katika kaunti hizo nane.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Yusuf Hassan aishinikize serikali...

TAHARIRI: Hatua iliyopigwa na Waziri kuhusu kandanda inatia...

T L