• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 10:11 AM
DOUGLAS MUTUA: Serikali iipe umuhimu afya ya akili ya wanajeshi wetu

DOUGLAS MUTUA: Serikali iipe umuhimu afya ya akili ya wanajeshi wetu

NA DOUGLAS MUTUA

NIMETAFAKARI kuhusu hatua ya Rais wa Kenya, Dkt William Ruto, kuwaombea wanajeshi wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF) walioenda vitani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kinyume na Wakenya wengi, sikuajabia Rais kutia dua; ni jukumu letu sote tunaomwamini Mungu kumnyenyekea kila wakati, tuwe watawala au kina yakhe.

Tumewahi kumshuhudia Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akiombea mvua, marehemu Daniel arap Moi akinyenyekea kanisani na viongozi wa mataifa mengine wakiswali misikitini.

Maombi ya Dkt Ruto yalinipa tafakuri na masikitiko kwa sababu Kenya imetokea kutelekeza afya ya akili ya wanajeshi wake wanaoenda kutumika nje. Nilijiuliza iwapo tutawatunza vyema wakirejea nchini baada ya kuhudumu huko ambako wataongoza wenzao wa Burundi, Uganda na Sudan Kusini kupambana na waasi wa M23.

Japo KDF wamehudumu ndani na nje ya bara la Afrika kwa miaka mingi kutokana na utaalamu wao, suala la afya ya akili lilijitokeza walipoenda kukabiliana na magaidi wa Al-Shabaab nchini Somalia.

Miaka ya tisini, wanajeshi wetu walipotumika Timor Mashariki, Namibia, Croatia, Macedonia na Angola, walizorejea nazo ni sifa za ujasiri na mafedha ya kuhusudiwa!

Wakati huo ilichukuliwa kawaida kwa mwanajeshi aliyebahatika kutumwa nje ya nchi chini ya Umoja wa Mataifa kutajirika.

Hatukusikia chochote kuhusu maradhi ya akili, kama vile msongo wa mawazo, ambayo husababishwa na unyama wanaoshuhudia, au wenyewe kushiriki, wakiwa vitani.

Mambo yalibadilika walipoanza kurejea kutoka Somalia, baadhi yao wakiwa na majeraha yaliyowalemaza na wengine wakiachishwa kazi kwa kudhoofikiwa na afya ya akili.

Mpaka sasa kuna wengi wanaoteseka kimya kimya, baadhi yao wamevuruga familia zao kiasi cha kuzitawanya na hata kuwajeruhi jamaa na marafiki. Wapo waliojitia kitanzi pia. Binafsi ninaamini tatizo la afya ya akili limekuwapo KDF muda wote huu, tangu miaka ya tisini, ila kawaida yetu Waafrika miaka ile tukizembea kutambua baadhi ya maradhi.

Mwanajeshi akitenda unyama siku hizo aliaminika kuwa mkali kutokana na uzoefu wake kazini, hasira zake zikichukuliwa kuwa ushujaa na kuachwa atende alivyotaka badala ya kusaidiwa.

Namkumbuka mmoja wa mababu zangu aliyetumika nchini Burma wakati wa Vita vya Pili vya Dunia; ghafla angepiga suluti na kuanza kutembea kwa mwendo wa kijeshi! Akijikunja kwa umbo la mviringo, kujigaragaza na kufanya maonyesho mengine ya mbinu za kivita. Alipoamka kwa mguu wa kushoto na kuona cha kwako akitake ndio basi! Maskini hukuwa na chaguo ila kukisalimisha. Aliwatesa na kuwaudhi wengi. Ajabu akidi ni kwamba muda mfupi baadaye angejutia matendo yake na kulia sana, ila bila kuomba msamaha, na ungalimuuliza kunani hungalipata jibu. Labda upigwe kibao! Wakuruba wake walisema hakujutia tu vitendo vyake vya wakati huo bali pia mateso aliyopata, maovu aliyotenda na damu ya watu aliyoshuhudia ikimwagika vitani. Aliondoka duniani bila jaribio lolote la kumtibu kufanywa. Huo ni mfano mmoja tu, kuna maelfu ambao wameingia kaburini kimyakimya ila na madhila tele.

Hivi majuzi KDF ilinadi hospitali yake mpya na ikasifia uwezo wake wa kuwashughulikia wagonjwa wa maradhi ya akili, lakini bado nadhani haitoshi.

Ukiunga wanajeshi wanaorejea kutoka Somalia na watakaotoka DRC, ni rahisi kukadiria kwamba hospitali hiyo ni ndogo, tena matabibu ni wachache mno.

Tunahitaji huduma hizo kwenye hospitali nyingi hivi kwamba mashujaa wetu wakirejea watatibiwa kama dharura, wasisubiri kwenye foleni.

Huku akiendelea kuahidi kuboresha huduma kwa wananchi katika utawala wake mpya, Rais Ruto anapaswa kuipa kipaumbele afya ya akili ya KDF.

Akifanya hivyo, afya ya akili itaanza kushughulikiwa kwa mazingatio yanayostahili nchini.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Hatua iliyopigwa na Waziri kuhusu kandanda inatia...

WANDERI KAMAU: Afrika imedhihirisha ina uwezo wa kutatua...

T L