• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
TAHARIRI: Hawakustahili kufa namna ile katika ajali ya basi mtoni Kitui

TAHARIRI: Hawakustahili kufa namna ile katika ajali ya basi mtoni Kitui

KITENGO cha UHARIRI

Ajali ya basi katika Mto Eziu, eneo la Mwingi, Kitui mnamo Jumamosi inasikitisha na kuzua maswali mengi.

Hakika ilikoroga nyongo kutazama video ya basi hilo lililokuwa limebebea wanakwaya wakielekea harusini, kupoteza mwelekeo na kubingiria mtoni wakati lilipokuwa likijaribu kuvuka mto uliofurika.Kufikia wakati tulipokuwa tukienda mitamboni jana, zaidi ya miili 22 ilikuwa ishaopolewa kutoka mtoni huku 35 wakiwa bado hawajulikani waliko.

Ni ajali ambayo wengi wamelaumu makosa ya kibinadamu kwa dereva kuhiari kuvuka mto ambao ulikuwa na mafuriko kama ule. Abiria pia wamelaumiwa kuabiri chombo ambacho kilikuwa kinakodolewa na hatari kama ile. Lakini kuwalimbikizia lawama itakuwa kuepuka kuangalia kwa uhalisia aliyeangusha wakazi wa eneo hilo la Kitui.

Kwa taifa ambalo rais wake alitangaza juzi tu kwamba linashikilia nafasi ya sita kwa utajiri Afrika, hakika hakupaswi kuwa na sehemu yoyote ya nchi hii ambayo inakosa muundomsingi muhimu kama daraja namna ile.Kwa kweli, kwa kuangalia sehemu ile, unaona aina fulani ya ujenzi wa daraja uliokuwa unafanywa na kukwama.

Na hapo ndipo hali inajitokeza kama ilivyo sehemu zingine za nchi: wananchi wanalilia huduma fulani kwa miaka na mikaka, wanasiasa wanaahidi kutekeleza kwa miaka na mikaka, hatimaye kandarasi inapewa kampuni fulani na ujenzi unaanza hivyo kuzua matumaini, kisha jambo fulani linatokea — mara nyingi hivi mwanakandarasi na idara husika wanakosana, pesa zinaisha au kutoweka na mradi unakwama.

Wakazi wanabaki pale pale na shida zao.Ama kweli kama kuna mkasa ambao unaelezea jinsi hali ya maisha katika taifa hili ilivyo, basi ni huu. Takriban kila kaunti utakayoenda, utakuta uhitaji fulani wa muundomsingi ambao ni muhimu kiasi kwamba wakazi wanahatarisha maisha yao kila siku kwa kukosekana kwa huduma hiyo.

Lakini wanasiasa wetu ndio hao wanazidi kupiga siasa kila siku. Serikali zetu, ya kitaifa na za kaunti ndio hizo zinatumia mabilioni ya pesa kwa ziara na mambo mengine ambayo yanaendeleza maslahi ya kibinafsi.

Abiria wale wanakwaya kule eneo la Mwingi, Kitui, waliponzwa na uongozi mbaya unaojitia hamnazo huku mamia ya watu wakihatarisha maisha yao kila siku kushiriki hafla za kimsingi za kimaisha kama kwenda harusini.

You can share this post!

WANTO WARUI: Wasimamizi wa shule za sekondari wapewe...

WANDERI KAMAU: Jamii zirejelee misingi ya malezi bora...

T L