• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Kenya iige mfano wa Tanzania kuuza Kiswahili kimataifa

TAHARIRI: Kenya iige mfano wa Tanzania kuuza Kiswahili kimataifa

NA MHARIRI

HAPO Jumanne Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilitia saini makubaliano na taasisi tatu za elimu ya juu katika mataifa ya Afrika kuhusu ufundishaji wa Kiswahili.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa aliambia bunge la Tanzania kwamba chuo hicho cha serikali kimetia saini makubaliano na Chuo Kikuu cha Joachim Chissano cha Msumbiji, Chuo Kikuu cha Port Harcourt cha Nigeria na Chuo Kikuu cha Addis Ababa, Ethiopia ya kukiwezesha kufundisha Kiswahili katika vyuo hivyo.

Hatua hii inatokana na hatua ya kutawazwa kwa Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kuendeshea shughuli katika Umoja wa Afrika (AU).

Tayari Kiswahili kimeteuliwa kuwa lugha rasmi ya kuendeshea shughuli na vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).Baraza la jumuiya hiyo kuhusu Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo (SCESTCS) pia lilipitisha muafaka wa kufanya Kifaransa kuwa lugha rasmi katika EAC.

Lugha ya Kiingereza ndiyo imekuwa ikitumiwa kama lugha rasmi katika shughuli za EAC.

Aidha, Kiswahili hutumika kama lugha rasmi katika Jumuiya ya Ustawi wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Walimu 1,130 wa Kiswahili kutoka Tanzania wametumwa kufundisha lugha hiyo katika mataifa mbalimbali ya kigeni, yakiwemo Afrika Kusini, Uganda, Poland, Ujerumani na Uingereza.

Mnamo Novemba 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), liliteua Julai 7, kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Ulimwenguni.

Jumuiya ya EAC itaandaa maadhimisho ya kwanza ya siku hiyo katika kisiwa cha Zanzibar mnamo Julai 7, 2022. Hafla hiyo itasimamiwa na Tume ya Kiswahili Afrika Mashariki (EAKC).

Hatua kadha zilizochukuliwa za Afrika pamoja na Dunia katika kukweza hadhi ya Kiswahili imeleta msisimko mkubwa kwa wapenzi wa lugha hii ashirafu.

Hata hivyo, taifa jirani la Tanzania linaonekana kuwa katika mstari wa mbele kuchukua hatua madhubuti na za kimakusudi kusambaza Kiswahili.

Katika kufanya hivi, Tanzania inatafutia wasomi wake wa Kiswahili ajira katika masoko ambayo yamejitokeza barani Afrika na kwingineko ulimwenguni.

Inasikitisha kwamba taifa la Kenya limeachwa nyuma.

Tunafaa kuchuma nafuu ya fursa zilizojitokeza kutafutia wataalamu wetu nafasi za ajira nje ya taifa letu.

Serikali ya Kenya inafaa kuiga mfano wa Tanzania na kutafutia raia wake fursa hizi.

Itakuwa rahisi iwapo miafaka ya namna hii itafanywa katika ngazi ya serikali kwa serikali ilivyofanya Tanzania badala ya watu binafsi.

Kenya ina wataalamu waliobobea katika lugha ya Kiswahili na umefika wakati kwetu kuchangamkia fursa ya kubidhaishwa kwa lugha hii ashirafu ili kuchumia watu wetu riziki.

  • Tags

You can share this post!

Mtafaruku Sonko akipigwa breki kuwasilisha stakabadhi kwa...

ZARAA: Afichua siri ya jinsi alivyofaulu katika kilimo cha...

T L