• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mtafaruku Sonko akipigwa breki kuwasilisha stakabadhi kwa IEBC

Mtafaruku Sonko akipigwa breki kuwasilisha stakabadhi kwa IEBC

ANTHONY KITIMO NA BRIAN OCHARO

KULIKUWA na kizaazaa jana Jumanne katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Kaunti ya Mombasa, wakati jaribio la aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kuwasilisha stakabadhi zake za uwaniaji ugavana Mombasa liligonga mwamba.

Mamia ya wafuasi wa Bw Sonko walianza kuwasili mapema karibu na afisi hiyo iliyoko katika mtaa wa Kizingo wakimsubiri.

Polisi walikuwa wamezingira eneo hilo kuepusha uwezekano wowote wa fujo.Msafara wa Bw Sonko uliwasili dakika chache baada ya saa nane mchana, akafika mbele ya afisa mkuu wa IEBC, Bi Swalhah Yusuf, saa nane na dakika 19 ambapo alikaribishwa vyema na stakabadhi zake zikaanza kukaguliwa.

Alikuwa ameandamana na mawakili wake na mgombea mwenza wake ambaye pia ni Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo.

Mvutano ulianza ilipobainika kuwa baadhi ya stakabadhi zake hazikuwa zimepigwa muhuri na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), lakini hilo likasuluhishwa wasaidizi wake walipoleta stakabadhi zenye muhuri.

Baadaye, Bi Yusuf aliwaarifu kuwa, hakuwa amepokea mawasiliano yoyote kwamba, mahakama ilibatilisha uamuzi wa tume kutoidhinisha wanasiasa waliobanduliwa mamlakani kwa sababu za kimaadili.

Bi Yusuf alisema, kwa msingi huo, maafisa wa IEBC hawana budi ila kuendelea kufuata msimamo uliotangazwa na mwenyekiti, Bw Wafula Chebukati, kuwa wanasiasa aina hiyo hawastahili kuwania wadhifa wowote wa umma.

Ilibidi maafisa wa polisi waitwe ndani ya ukumbi huo na kuwazingira maafisa wa IEBC wakati hasira zilipoonekana kupanda upande wa kikosi cha Bw Sonko.

Bw Sonko aliyepewa tikiti ya Wiper alisisitiza alikata rufaa katika Mahakama ya Juu dhidi ya uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Nairobi na Seneti kumbandua mamlakani kwa hivyo anastahili kuruhusiwa kuwania.

Mbali na hayo, alisisitiza kuwa, mahakama Jumatatu ilibatilisha kwa muda maagizo ya IEBC kuzuia waliong’olewa mamlakani kuwania viti.

Baada ya thibitisho kupokelewa kwamba, kuna rufaa katika Mahakama ya Juu, Bi Yusuf alisema saa za kazi ni hadi saa kumi kwa hivyo hangeweza kuwahudumia akisema muda rasmi wa kutathmini wagombeaji umepita.

Kufikia wakati wa kwenda mtamboni, Bw Sonko alikuwa bado amekataa kuondoka katika ukumbi huo akitaka kukabidhiwa cheti cha uwaniaji.

Awali, IEBC ilimwidhinisha aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, kuwania ugavana Mombasa kupitia chama cha UDA.

Akizungumza katika mikutano ya hadhara baada ya kupewa cheti na IEBC, Bw Omar aliahidi kuleta uongozi bora utakaofaidi wakazi wa Mombasa.

Alikosoa utawala wa Gavana Hassan Joho, akidai umesababisha wafanyabiashara kupata hasara kwa sababu ya kutozwa ada chungu nzima.

“Sisi tuna imani tunaweza kugeuza uchumi wa jiji hili,” akasema.

Alikuwa ameandamana na wagombeaji viti wengine wa UDA akiwemo Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, na mgombeaji ubunge Mvita, Bw Omar Shallo.

Walipigia debe azma ya Naibu Rais William Ruto kurithi kiti cha Rais Uhuru Kenyatta, wakisema wanaamini ana uwezo wa kutatua changamoto zinazokumba wananchi hasa wa daraja la chini kimaisha.

  • Tags

You can share this post!

UDA bado ndio kusema Mlima Kenya – Gachagua

TAHARIRI: Kenya iige mfano wa Tanzania kuuza Kiswahili...

T L