• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
TAHARIRI: Kuongeza ujira ni sawa, ila uchumi uboreshwe

TAHARIRI: Kuongeza ujira ni sawa, ila uchumi uboreshwe

NA MHARIRI

HATUA ya serikali ya kutangaza nyongeza ya mshahara wa chini ya asilimia 12 ni nzuri ikizingatiwa kuwa gharama ya maisha imepanda na kulemea Wakenya wengi.

Ni zawadi ya Leba Dei ambayo wafanyakazi wa nchi wamekosa kwa muda.

Hii ilikuwa mara ya kwanza serikali kuongeza mishahara ya chini katika kipindi cha miaka minne.

Akitangaza nyongeza hiyo, Rais Kenyatta alisema kuwa hiyo ni njia ya kutambua juhudi na bidii ya wafanyakazi wanaoinua uchumi wa nchi na kuwawezesha kukabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha kunakosababishwa na janga la corona.

Japo hatua ya serikali ni ya kupongezwa, ukweli mchungu ni kwamba huenda isilete mabadiliko kwa maisha ya Wakenya.

Hii ni kwa sababu waajiri wanaopaswa kutekeleza nyongeza hiyo wanakabiliwa na hali ngumu ya kudumisha biashara zao kutokana na mazingira ambayo kwa njia moja, serikali imeweka.

Itakuwa bora zaidi serikali ikibuni mazingira ya kufufua biashara ili ziajiri Wakenya wengi.

Katika kipindi cha miaka miwili ambacho corona iliathiri uchumi, Wakenya zaidi ya 2 milioni walipoteza kazi zao na kusema kweli, wanahangaika huku gharama ya bidhaa za kimsingi ikiendelea kuongezeka.

Kwao na familia zao, nyongeza ya mishahara ambayo serikali ilitangaza jana haina maana kwao.

Alivyosema Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri, Jackline Mugo, kwenye hotuba yake ya kuadhimisha Leba Dei mwaka huu, serikali inapaswa kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini ili kuongeza kasi ya kufufua uchumi.

Ikiwa haitaweka sera za kuboresha uchumi, itakuwa vigumu kwa waajiri kutekeleza nyongeza ya mishahara na kuna uwezekano wa wafanyakazi wengi wa sekta ya kibinafsi kupoteza ajira.

Huu ndio ukweli mchungu ambao Wakenya, wakiwemo walioshangilia tangazo la serikali, wanapaswa kuwa tayari kukabiliana nao.

Kuimarika kwa uchumi kutafanikishwa na sera za serikali za kuvutia wahusika wote katika biashara.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona wapepeta Mallorca na kupaa hadi nafasi ya pili...

Serikali yaagiza shule kufunguliwa Baringo

T L