• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
TAHARIRI: Maafisa wapya wahakikishie raia usalama tosha

TAHARIRI: Maafisa wapya wahakikishie raia usalama tosha

NA MHARIRI

SERIKALI kupiti wizara ya Usalama mnamo Ijumaa ilifanya mageuzi na kuwaondoa maafisa wote wanane waliokuwa wakisimamamia maeneo.

Mageuzi hayo yalitokana na ahadi ya serikali ya Kenya Kwanza kwamba ingeweka watu wanaoelewa sera zake.

Kwamba maafisa walioondolewa walikuwa wakifanyia kampeni mwaniaji urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga.

Fikira hizi zikawa ukweli kwa baadhi, lakini si kila mmoja wa wasimamizi hao wanane alikuwa na mapendeleo hayo.

Sheria iko wazi kwamba afisa wa umma anapaswa kuunga mkono na kuchukua maagizo kutoka kwa serikali iliyo mamlakani.

Wasimamizi hao wa maeneo huwa na majukumu muhimu ya kuoanisha shughuli za serikali ya kitaifa na yale ya Kaunti.

Jukumu la usalama ni la serikali ya kitaifa pekee. Mmoja wa maafisa walioleta utulivu mkubwa eneo na Rift Valley, Bw Mohammed Maalim ni kati ya waliorejeshwa katika Afisi ya Rais.

Hata kabla mrithi wake hajakalia kiti cha ofisi, tayari majangili wamevamia na kuua watu. Shambulio hilo pia limeathiri watu kadhaa ambao walilazimika kutoroka kwao.

Hali hii ya mashambulio yafaa kudhibitiwa kwa haraka, sio tu katika Bonde la Kerio, bali kila pembe ya nchi yetu.

Jukumu kubwa la serikali kupitia wizara ya Usalama ni kuwalinda wananchi na mali zao. Usalama unachangia maendeleo. Hakuna mwekezaji anayeweza kuweka mamilioni katika eneo ambalo halina usalama.

Biashara hufungwa mapema, walimu, wahudumu wa afya na watoaji huduma wengine kutoka maeneo mengine hukataa kutumwa huko. Tumeshughudia hali hii Kaskazini Mashariki mwa nchi ambako hutokea mashambulizi ya kila mara, yanakumbwa na uhaba mkubwa wa walimu.

Serikali ina uamuzi wa kufanya mageuzi katika idara zake kama njia ya kuimarisha utendakazi na utoaji huduma. Lakini mageuzi hayo hayafai kufanywa kwa hisia, bali yawe yatakayoendeleza kuwepo kwa usalama, utulivu na kuhakikishia kila mtu nchini kuwa shughuli za serikali zitaimarika.

Katika kipindi hiki ambapo wananchi wanapambana na ugumu wa maisha, jambo la mwisho wanalotarajia ni kusikia kuwa hawako salama. Serikali ifanye hima na kutuma maafisa wa usalama kukabiliana na wanaohusika na mashambulizi. Hili ni jukumu lisiloweza kuepukika.

Wakuu wapya wa kushirikisha serikali, yawapasa waingie kazini mara moja na kutambua kuwa walipandishwa vyeo kwa vile serikali ina imani na utendakazi wao. Kusiwe na visingizio vyovyote kwa wao kukosa kuwalinda raia na mali zao.

  • Tags

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mbunifu katika ufundishaji

Aston Villa washiba sifa za kocha wao Unai Emery baada ya...

T L