• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mbunifu katika ufundishaji

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mbunifu katika ufundishaji

Na CHRIS ADUNGO

UKIITIKIA wito wa kuwa mwalimu, basi fahamu kuwa taifa lote la kesho linakutazamia.

Jamii nzima huwa imekuamini na mtoto ambaye mzazi wake amekuachia shuleni. Kwa sababu hiyo, matarajio ya kila mtu kwako huwa ni ya kiwango cha juu sana.

Falsafa hii imekuwa mwongozo madhubuti kwa mwalimu John Kilonzo ambaye sasa anafundisha Kiswahili, Hisabati na somo la Jamii katika shule ya msingi ya Missions of Hope International Boys Boarding & Mixed Day iliyoko Ndovoini, Kaunti ya Machakos.

Kwa mtazamo wake, wanafunzi humwamini sana mwalimu aliye na ufahamu mpana wa masomo anayofundisha. Hivyo, mwalimu bora anastahili kufanya utafiti wa kina katika somo lake na kuchangamkia masuala yote yanayofungamana na mtaala.

“Anapswa pia kuelewa uwezo, changamoto na mahitaji ya msingi ya kila mwanafunzi. Ajitahidi kuhudhuria vipindi vyote, atoe mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi, arejeshe masahihisho ya kazi zao mapema na awape matokeo ya majaribio ya mitihani kwa wakati unaofaa,” anasema.

“Mbali na kuwa mnyumbufu wakati wa kuandaa vipindi na mbunifu katika uwasilishaji wa masomo yake, inampasa pia mwalimu awe na ujuzi wa kutumia nyenzo anuwai za ufundishaji zitakazowaamshia wanafunzi ari ya kuthamini masomo na kukuza vipaji vyao,” anaelezea.

Kilonzo alilelewa katika eneo la Masii, Kaunti ya Machakos. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa marehemu Bw Michael Ndumbu na marehemu Bi Jane Kanini.

Alisomea katika shule ya msingi Mikuyuni iliyoko Masii (2000-2008) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Mumbuni Boys, Machakos (2009-2012).

Japo matamanio yake yalikuwa kujitosa katika taaluma ya udaktari, alihiari kusomea ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Lanet, Kaunti ya Nakuru (2014-2016).

Uamuzi wa kujibwaga katika ulingo wa ualimu ulikuwa zao la kuchochewa zaidi na Bi Florence Muthoka Kyule na Bi Rose Mbithi waliompokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya msingi. Mwingine aliyemhimiza pakubwa kusomea ualimu ni aliyekuwa Naibu Mwalimu Mkuu wa shule ya upili ya Mumbuni Boys, Bw Peter Mwololo.

Kilonzo alipokea mafunzo ya nyanjani katika shule ya msingi ya Kariba iliyoko Nakuru mnamo 2015 na akaajiriwa na shule ya msingi ya Blessed Small Angels Academy jijini Nairobi mnamo 2016. Alihudumu huko kwa miaka mitatu kabla ya kuhamia Missions of Hope International Boys Boarding & Mixed Day mnamo 2018.

Anaungama kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote hutegemea pakubwa mtazamo wake kwa masomo anayofundishwa na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Uzoefu wake katika ufundishaji wa Kiswahili, Hisabati na somo la Jamii umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kushauri, kuelekeza na kuhamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

  • Tags

You can share this post!

Nzi kufa kidondani si haramu (sehemu ya 3)

TAHARIRI: Maafisa wapya wahakikishie raia usalama tosha

T L