• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
TAHARIRI: Mageuzi katika polisi yasiingizwe siasa

TAHARIRI: Mageuzi katika polisi yasiingizwe siasa

NA MHARIRI

JUHUDI za kutakasa huduma ya polisi ambazo zimeanzishwa na serikali ya Rais William Ruto hazifai kuingizwa siasa.

Na hata Mheshimiwa Rais mwenyewe hafai kuziingiza siasa japo ana haki ya kueleza Wakenya anachofanya kuwahakikishia usalama wao.

Hilo ni jukumu lake na ameanza kulitekeleza.

Hakuna asiyesadiki kuwa watu wamekuwa wakitekwa nyara kiholela, kuuawa na kutoweka. Kufikia sasa baadhi yao hawajawahi kupatikana.

Kufikia jana Jumamosi, maafisa wanne wa kitengo kilichovunjwa walikuwa wametiwa mbaroni na tunataka kuamini kuna sababu za kutosha kufanya hivyo na kwa nia njema.

Ikiwa imebainika na kuthibitishwa bila chembe ya shaka kwamba ni kitengo hicho cha Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu kilichovunjwa wiki jana ambacho kilikuwa kikihusika na uhayawani huu wa ukiukaji wa haki za binadamu, kulikuwa na kila haki ya kuvunjwa mradi tu kingine kipya kisiundwe kuendeleza ukatili huo au mbaya zaidi.

Kila wakati hatua kama hizi zinapochukuliwa, baadhi ya wanasiasa huwa wanaanza kuingiza cheche za siasa bila kujali kwamba kuna watu wanaolilia kupata haki baada ya kupoteza wapendwao wao.

Hata hivyo, hadi pale watakapopatikana na hatia kupitia mchakato wa kisheria, maafisa waliokamatwa wangali washukiwa, na washukiwa wako na haki zao na zinafaa kuheshimiwa.

Ili juhudi hizi ziweze kuwa na athari kwa jamii pana ya Wakenya, zinafaa kupanuliwa hadi kwa vitengo na idara zingine za Huduma ya Polisi.

Hivyo basi, utakaso unaoendelea katika DCI unafaa kufanywa kwa Idara ya Trafiki ambayo, kulingana na ripoti kadhaa, imekolewa na ufisadi ambao, umetajwa kama moja kati ya vyanzo vya ajali za barabarani.

You can share this post!

Dortmund na Bayern watamba katika michuano yao ya Bundesliga

Uozo katika Jubilee waanza kufichuliwa

T L