• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
TAHARIRI: Mageuzi yajayo katika HELB yafanywe kwa umakinifu

TAHARIRI: Mageuzi yajayo katika HELB yafanywe kwa umakinifu

NA MHARIRI

SERIKALI imeeleza mpango wa kufanyia marekebisho mfumo mzima wa kufadhili elimu ya wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya kiufundi.

Katika mpango huo, mojawapo ya mabadiliko makuu yanayolengwa ni kwamba, wanafunzi wanaotoka katika familia zinazojiweza kifedha wasiwe wakifadhiliwa katika elimu ya juu.

Maafisa serikalini wamesema wazi kuwa, lengo ni kuhakikisha fedha chache zilizopo zinatumiwa kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia zisizojiweza kifedha.

Msingi unaotumiwa hapa ni kwamba, kuna wanafunzi wengi ambao wazazi au walezi wao huwa na uwezo wa kugharimia masomo yao yote katika shule za kifahari za msingi na upili ilhali wanapofika katika vyuo vikuu, wao pia wanataka kupewa ufadhili na serikali.

Ijapokuwa kuna uwezekano kwamba serikali ina nia njema ya kuepusha utumizi bora wa fedha za umma, ni sharti kuwe na tahadhari ili mwelekeo huu usiwaache nje wanafunzi walio na mahitaji.

Haitakuwa busara kutumia kigezo kwamba mwanafunzi alisomea shule ya kibinafsi ya msingi na upili, basi kwa hivyo asipewe ufadhili katika chuo kikuu au taasisi yoyote ile ya elimu ya juu.

Kuna watoto wengi ambao hupokea ufadhili wa wahisani kusomea katika shule nzuri za kibinafsi za msingi na upili.

Kutakuwa na hatari ya watoto aina hii kuchukuliwa kwamba wanatoka katika familia tajiri, kisha wanyimwe ufadhili katika vyuo vikuu ilhali ukweli ni kwamba wanahitaji kuendelea kusaidiwa.

Mbali na hayo, kuna wengine wengi ambao wazazi wao hung’ang’ana mno kuwasomesha katika shule za msingi na upili za kibinafsi hata kama mapato yao ni madogo.

Kuwepo kwa Hazina ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) huwa ni afueni kwa kikundi hiki cha familia kwani ule mzigo mzito wa kuendeleza elimu ya watoto wao hupunguzwa.

Ni sharti wadau wote wanaohusika katika kutoa sera mpya za kufadhili wanafunzi katika vyuo vikuu wawe makini ili kuepusha madhara kwa familia na vijana.

Iwapo kuna hitaji la kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopokea mikopo hii, hatua hiyo ifanywe kwa busara bila kutumia mbinu ambazo zinaweza kuwadhulumu maelfu ya wanafunzi wenye mahitaji ya kifedha.

Vilevile, itakuwa vyema kama serikali itatafuta njia mwafaka ya kuhakikisha kuwa wanaopokea mikopo hii wanailipa kwa muda unaostahili.

Kuna wengi ambao huwa wameajiriwa au kujiajiri ilhali huapa kwamba hawatawahi kulipa mikopo waliyopewa.

Hii ni mojawapo ya sababu zinazofanya hazina ya HELB kukauka kila kukicha.

  • Tags

You can share this post!

Jambazi ‘msaliti’ aomba atumikie kifungo cha nje

Maswali chungu nzima baada ya vigogo wa Azimio kususia...

T L