• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Msimu wa tohara ni wakati mzuri kukoleza maadili mema kwa vijana

TAHARIRI: Msimu wa tohara ni wakati mzuri kukoleza maadili mema kwa vijana

NA MHARIRI

JAMII mbalimbali nchini zinaendelea na sherehe za kupasha tohara watoto wavulana wakati huu wa likizo hii ndefu ya Desemba.

Ilivyo kawaida, mbwembwe za kila aina hushuhudiwa wakati wa kutekelezwa kwa desturi hii muhimu sana muhimu ya kitamaduni.

Ni kipindi hiki ambapo marika ya wavulana hutambuliwa rasmi katika jamii, na hata kupewa majina ya kishujaa.

Kando na jina la rika, wavulana hao walitunukiwa pia zawadi kemkem na wazazi wao pamoja na wanajamii wa koo zao za karibu.

Isitoshe, wavulana hao huchukuliwa sasa kama vijana waliokomaa kiumri baada ya kupitisha jandoni. Kitamaduni ukomavu huo ulimaanisha kijana sasa angehamia katika kijumba chake kidogo kwani hangeruhusiwa tena kulala katika nyumba ya wazazi.

Ukomavu pia ulimpa fursa ya kuhusishwa katika vikao vya watu wazima kujadili masuala ya familia yao na jamii kwa jumla.

Yote tisa, msimu huu wa tohara ndio wakati ambapo ushauri nasaha na mafunzo ya kijamii hufunzwa vijana hao kwa kina.

Kipindi hiki ni fursa nzuri kabambe ya kukoleza maadili mema miongoni mwa wavulana hao, hususan kwa kuzingatia hatari ya janga la ukimwi ambalo limeanza kuinuka tena nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde zilizotolewa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Ulimwenguni hapa nchini, Kenya imeshuhudia ongezeko la maambukizi kwa asilimia 7.3 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Kulikuwa na ongezeko la maambukizi ya virusi vya HIV – vinavyosababisha ukimwi – kutoka visa 32,027 hadi 34,540.Katika takwimu hizo, asimilia 52 ya maambukizi ni miongoni mwa vijana wachanga walio kati ya miaka 15-24.

Ni hali ya kutia wasiwasi kwani ni taswira inayoashiria kuwa vijana wachanga hawashiriki tu ngono bali wanakula fuska kiholela pasipo kuzingatia kinga.

Ni msemo mamboleo mitaani kwamba vijana wa siku hizi wanaogopa zaidi kushika mimba kuliko kupata Ukimwi, ndiposa dawa za kuzuia mimba zinauza kama moto kichakani.

Maambukizi haya mapya ni hatari mno na yanatishia kurudisha nyuma jitihada nyingi ambazo Kenya imepiga kushusha viwango vya ukimwi hadi asilimia 4.9 kitaifa.

Sherehe za tohara ni wakati mwafaka sana kwa serikali ya kitaifa na kaunti kutumia kama jukwaa la kueneza ujumbe vijana wajiepushe na ngono kiholela kwani ni hatari kwa maisha.

  • Tags

You can share this post!

Talaka ya Jubilee na ODM sasa yaiva

MAPISHI KIKWETU: Saladi ya kuku, maembe na tango

T L