• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:37 AM
Talaka ya Jubilee na ODM sasa yaiva

Talaka ya Jubilee na ODM sasa yaiva

NA BENSON MATHEKA

NDOA ya kisiasa iliyoleta pamoja vyama 26 ili kuunda Azimio la Umoja-One Kenya inaonekana kuvunjika baada ya ripoti kwamba Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta anapanga kujiuzulu kama mwenyekiti wa Baraza Simamizi la muungano huo.

Wandani wa karibu wa Rais Kenyatta walisema kwamba muungano huo utaita mkutano wakati wowote ambapo rais huyo wa nne wa Kenya atajiuzulu na kuacha uongozi wa Azimio katika mikono ya Raila Odinga.

Bw Odinga alikuwa mgombeaji urais wa muungano huo katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kujiuzulu kwa Bw Kenyatta kutaashiria mwisho wa uanachama wa chama chake cha Jubilee katika Azimio na vyama vingine vinaweza kufuata mkondo huo ikizingatiwa kuwa mkataba wa muungano huo umevifungulia mwanya wa kuhama.

Wachanganuzi wa siasa wanasema sio sadfa kwamba hatua ya Bw Kenyatta inajiri wakati vyama tanzu viko huru kuhama Azimio kwa kuwa mkataba wa muungano huo unavifungua kuhama miezi mitatu baada ya uchaguzi.

“Ni Bw Kenyatta ambaye alitumia mamlaka yake akiwa rais kuunganisha vyama vya kisiasa nyuma ya Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Hivyo basi, kujiondoa katika muungano huo kutamaanisha utasambaratika,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Geff Kamwanah.

Baadhi ya vyama tanzu vya muungano huo ni ODM cha Bw Odinga, Narc Kenya cha Martha Karua ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga, Wiper cha Kalonzo Musyoka, Kanu cha Gideon Moi, Narc cha aliyekuwa gavana wa Kitui Charity Ngilu, DAP Kenya kinachohusishwa na aliyekuwa waziri Eugene Wamalwa, Devolution Empowerment Party (DEP), United Party of Independent Alliance (UPIA), Kenya Union Party (KUP) na Chama Cha Uzalendo (CCU) miongoni mwa vingine.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa kujiuzulu kwa Bw Kenyatta katika uongozi wa Jubilee na Azimio ni mwanzo wa mwisho wa muungano huo wakimtaja kama nguzo ya muungano huo.

Dkt Kamwanah anasema dalili kwamba talaka ya Azimio imeiva ni hatua ya waliokuwa wakereketwa wake kurushiana lawama kuhusu sababu za Bw Odinga kushindwa katika uchaguzi wa urais Agosti 9.

Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna amekuwa akisisitiza kuwa Jubilee inayoongozwa na Bw Kenyatta, haikusaidia Bw Odinga kupata kura ilizoahidi kutoka eneo la Mlima Kenya licha ya kutaka ‘minofu’ serikalini iwapo waziri mkuu huyo wa zamani angeshinda urais.

“Jubilee iliahidi mengi lakini haikuyatimiza licha ya kuwa ilitamani sehemu kubwa ya serikali iwapo Raila angeshinda,” Bw Sifuna aliambia wanasiasa wa Jubilee waliokosoa maamuzi ya ODM kuhusu nyadhifa bungeni.

Bw Musyoka ambaye alishawishiwa na Bw Kenyatta kumuunga Bw Odinga katika uchaguzi mkuu anasemekana kuanza kujipanga kugombea urais 2027 kivyake.

Wabunge na magavana wa vyama tanzu pia wamechangamkia serikali kwa kile kinachotazamwa kama juhudi za kuhakikisha kuna maendeleo katika maeneo yao ishara kuwa muungano uko matatani.

Duru zinasema ni baridi katika Azimio iliyofanya Bw Odinga kuacha baadhi ya vitendo vya kushinikiza na kukosoa serikali kama maandamano aliyopanga maeneo tofauti nchini.

Baadhi ya vyama tanzu tayari vimetangaza kuhama Azimio vikilalamikia kunyimwa haki na vyama vikubwa.

Mapema mwezi huu wa Desemba, kiongozi wa chama cha Kenya Union Party (KUP) Prof John Lonyangapuo alitangaza kwamba chama hicho kitaunga serikali ya Rais William Ruto huku akikitenga na mipango ya Bw Odinga ya kukosoa serikali.

“Vitendo vya hivi majuzi vya uongozi wa Azimio vimetuonyesha kuwa ahadi zilizotufanya kujiunga nao hazitatimizwa. Kwa sasa Azimio ndio tisho kuu kwa demokrasia, utawala wa sheria, na uwiano nchini,” alisema Prof Lonyangapuo.

You can share this post!

Kalonzo pabaya Ruto akiweka mikakati kupenya ngome yake

TAHARIRI: Msimu wa tohara ni wakati mzuri kukoleza maadili...

T L