• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
TAHARIRI: Ni hatari kupuuza shida za polisi

TAHARIRI: Ni hatari kupuuza shida za polisi

KITENGO cha UHARIRI

TAIFA kwa mara nyingine jana iliamkia habari kuhusu mauaji katika jamii yaliyosababishwa na afisa wa polisi bila sababu mwafaka kujulikana.

Katika kisa hicho, afisa wa polisi aliua watu sita akiwemo mke wake na raia wengine watano kabla kujitoa uhai.Visa hivi ambavyo vimekuwa vikitokea mara kwa mara, ambapo afisa wa polisi hutumia silaha yake kuangamiza familia yake na wengine anapohisi amekosewa vinafaa kutafutiwa suluhisho ya kudumu.

Kuna hatari kubwa kupuuza changamoto zinazokumba kikosi cha watu wanaokubaliwa kubeba silaha ambazo wao hutembea nazo kila mahali ndani ya jamii.Wadau wanaohusika katika masuala yanayohusu idara ya polisi pamoja na wataalamu wa kiakili hulaumu mahangaiko ya maafisa wa polisi nchini kuwa sababu ya baadhi yao kuchukua hatua za kinyama ikiwemo mauaji ya kiholela.

Licha ya serikali kutangaza awali kuwa mikakati imeekwa kusaidia maafisa wa polisi, inaonekana mipango hiyo haijafanikiwa kufua dafu kwa kiasi kinachoridhisha.Mapendekezo kama vile utoaji wa ushauri nasaha kwa polisi huenda ikawa yalipitishwa ila inavyoonekana, itakuwa muhimu kwa serikali na mashirika mengine husika kuwekeza rasilimali zaidi ili ibainike chanzo cha matatizo haya ni nini hasa.

Kuna wananchi ambao huamini kuwa idara ya polisi haijajitolea ipasavyo kuhakikisha kuwa maafisa wana utulivu wa kiakili wanapoendeleza majukumu yao ya kutoa usalama kwa umma.Dhana hii hutokana na jinsi mandhari ya kikazi na kimaisha ya polisi huonekana kuwa duni mno katika baadhi ya sehemu za nchi.

Kuanzia kwa vituo vya polisi hadi nyumba ambazo maafisa huishi, taswira inayoonekana kwa umma ni kuwa polisi wengi hasa wa ngazi za chini huteseka kimaisha.Haya yamezidishwa na hati za mishahara ya baadhi ya maafisa wa polisi ambazo husambazwa katika mitandao ya kijamii, ikionyesha jinsi wanavyopokea mishahara duni huku wengine wakidaiwa hata kukosa mishahara mwisho wa mwezi.

Ni taswira hii ambayo baadhi ya wananchi huamini husukuma idadi kubwa ya maafisa wa polisi kujitosa katika ulaji rushwa bila kujali ili wajiondoe katika maisha ya mateso, huku wale ambao hulemewa wakiaminika kuamua kujitoa uhai na kuangamiza yeyote anaowafanyia kosa bila kujali.

Serikali inahitajika ichukulie masuala haya kwa uzito zaidi, ishirikiane na wataalamu kutatua msingi wa matatizo haya.Chochote kile kitakachopatikana kuwa chanzo kitafutiwe suluhisho ya haraka wala ripoti za uchunguzi zisihifadhiwe ndani ya kabati jinsi ambavyo imekuwa mazoea kwa aina nyingine za uchunguzi zinazofanywa na serikali.

You can share this post!

OKA wapendekeza hukumu ya kifo kwa watu wafisadi

JUMA NAMLOLA: Tulitelekeza watoto wetu kwa muda mrefu, sasa...

T L